Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sidibe: Fei Toto, Yao ni balaa

Cheikh Sidibe Azam Beki wa kushoto wa Senegal anayekipiga Azam FC, Cheikh Tidiane Sidibe

Wed, 1 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Beki wa kushoto wa Senegal anayekipiga Azam FC, Cheikh Tidiane Sidibe ameweka wazi kwamba kama sio dili kubuma, pengine kwa sasa angekuwa kwa Wekundu wa Msimbazi.

Akizungumza na Mwanaspoti anasema viongozi wa Simba walisuasua kumsajili kabla ya Azam kutoa ofa na aliwasiliana moja kwa moja na meneja na kwa kuwa alikuwa akiifahamu ilikuwa rahisi kwenda huko kutokana na maslahi mazuri.

“Sikuona kama Simba wana uhitaji nami kwani licha ya kuzungumza nao niliwaelekeza kwa meneja wangu, lakini hawakufikia makubaliano ndipo nikatua Azam,” anasema Sidibe ambaye anakiri kwamba kama kuna beki wa kigeni anayejua kwenye Ligi Kuu Bara kwa sasa ni Yao Kouassi wa Yanga.

“Huyu Muivory Coast ni balaa,” anasema Sidibe kwenye mahojiano na Mwanaspoti na kuongeza kuwa alitua Azam akitokea Teungueth FC na amekuwa akianza kikosi cha kwanza cha Kocha Youssouph Dabo.

NDOYE AMVUTA TANZANIA

Anamtaja Msenegali mwenzake Malikou Ndoye aliyesajiliwa msimu uliopita na Azam ndiye aliyemfanya aitazame Ligi Kuu Bara. “Nilianza kwa kutazama mechi za Azam alikosajiliwa rafiki yangu. Nilivutiwa nayo lakini sikujua kama itatokea siku nitacheza kwenye ligi hii,” anasema Sidibe na kukiri ugali ndio chakula kilichompa changamoto tangu afike nchini na kuzitaja chapati ‘tapalapa’, wali kuku, nyama ndivyo anavyotumia kwani hata kwao vipo.

NAMBA TATU BORA, 10 PIA

Sidibe anasema licha ya kucheza beki namba tatu nafasi nyingine anazocheza ni namba 10 na winga: “Tofauti na namba tatu naweza kucheza pia kama winga na hata namba 10,” anasema kwa sasa yeye ni namba tatu bora katika Ligi Kuu Bara kwani bado hajaona wa kumshinda na ubora wake unatofautishwa na wengine kutokana na namna ya upigaji mipira ya kutenga.

“Ndio! Mimi ni namba tatu bora kwenye Ligi Kuu. Utofauti wangu na wengine ni vile navyoweza kupiga mipira ya kutenga ukilinganisha na mabeki wengine.”

FEI, YAO BALAA

Sidibe anasema bado anajifunza soka kutoka kwa waliomzidi akimtaja Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuwa ni mmoja wa wachezaji wazuri. Pia anamtaja beki wa kulia wa Yanga, Yao ndiye mchezaji mwenye nguvu na mbinu na amekuwa akimfuatilia kila mechi. “Feitoto anacheza vizuri sana. Ni mtu unayetamani kuona kila wakati akicheza kwa kuwa ni nafasi ninayoweza kuicheza pia. Najifunza vingi sana kutoka kwake.”

Kuhusu Yao anasema: “Bado sijawajua wachezaji wengi vizuri lakini huyu Muivory Coast wa Yanga anayecheza beki ya kulia Yao Kouassi ni mzuri, mwenye nguvu na mbinu za mpira. Ukimtazama kwa kawaida huwezi kudhani ndiye anayefanya haya uwanjani.”

JEZI NAMBA

Sidibe anasema anapenda kuvaa jezi namba 12 kwani anampenda beki wa kushoto raia wa Brazil, Marcelo Vieira da Silva aliyewahi kukipiga Real Madrid na sasa akiitumikia Fluminense ya Ligi Kuu Brazil. Alipofika Azam FC alikuta namba 12 tayari ina mtu akaambiwa achague kati ya namba 11 na 14 ambapo alipenda namba 14 akidai 11 hutumiwa zaidi na washambuliaji. “Naipenda sana jezi namba 12, ila nilikuta ina mtu, ndipo nilichagua 14, 11 hutumiwa na washambuliaji na mimi sichezi nafasi hiyo.

“Najifunza mengi kupitia kwa Marcelo kama anavyojilinda, anavyofanya mashambulizi ya kushtukiza kwa nidhamu, mikimbio hata namna ya kupokea mipira,” anasema.

TIMU YA TAIFA

Mchezaji huyo anasema hakuna ugumu wala urahisi kuitwa timu ya Taifa ya Senegal kwani ni kwa wachezaji wote wenye asili ya nchi hiyo bila kujali wanacheza nchi gani.

“Hakuna urahisi wala ugumu kwa sababu timu ya taifa ni kwa wote waishio Afrika au nje ya Afrika. Kocha akiona unamfaa atakuita lakini kama sio atampa nafasi mwingine. Mimi kutoitwa sioni kama ni shida na haijaniumiza kwani sio mara kwanza kuichezea timu ya taifa. Nimecheza hadi mashindano ya vijana ya U20, U23 pia hata Chan.”

BARA VS SENEGAL

Sidibe anasema tofauti ya ligi hizo mbili ipo eneo la mashabiki huku mashabiki wanapenda soka kuliko kwao, ingawa viwanja na namna ligi inavyochezwa ni sawa, mbinu na ubora wa timu ndio huamua matokeo.

“Hakuna utofauti mkubwa wa ligi ya hapa na Senegal viwanja na tunavyochezea na namna watu wanatumia nguvu ni sawa ila huku mashabiki wanapenda soka sana kuliko kule.

“Nimetazama baadhi ya mechi hata tulizocheza sisi naona kuna wakati uwanja unajaa tofauti kabisa kwetu sio hivyo,” anasema Sidibe ambaye aliwahi kuwa beki bora msimu wa 2020/21 akiwa na timu yake ya Teungueth FC na miongoni mwa wachezaji waliounda kikosi bora cha msimu huo.

HATASAHAU

Mchezaji huyo anasema yapo mengi amepitia katika soka yaliyompa nguvu na mengine kumkatisha tamaa, lakini hatasahau tukio la timu yake kubeba ubingwa wa michuano ya Chan 2023 kwani alikuwa mmoja wa nyota wa kikosi cha Senegal kilichochukua ubingwa na kuwa kwenye kikosi bora cha mashandano hayo.

“Yapo mengi ya kukatisha tamaa na kufurahisha ila siwezi kusahau tulivyokuwa mabingwa wa michuano ya Chan 2023 kule Algeria kwani niliisaidia timu yangu kupata ubingwa huo,” anasema Sidibe ambaye ni shabiki mkubwa wa mwanamuziki Daimond Platinumz akiupenda zaidi wimbo wake wa Enjoy

HAKUPENDA SHULE

Anasema licha ya kuwa baba yake alikuwa mwanasoka lakini alimhimiza kusoma ingawa yeye alipenda soka zaidi kuliko shule.

“(Hata hivyo) nimesoma masuala ya benki hadi kiwango cha digrii niliyoipata Chuo cha Cheikh Anta Diop de Dakar kilichopo Senegal na isingekuwa soka basi ningekuwa mtumishi wa benki.”

KIATU CHAKE

Nyota huyo ana jozi saba za viatu vya kuchezea mpira na zaidi ya tano za mazoezi huku akivaa namba 41, na anadai viatu anavyopenda ni vya Kampuni ya Nike. “Baba na kaka zangu walikuwa wakicheza mpira hivyo walininunulia, lakini kwa sasa natumia viatu vya Nike na huwa naviagiza Ulaya.”

Chanzo: Mwanaspoti