Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Si mchezo wametumia pesa nyingi za usajili kwenye soka

Pep Guardiola.jpeg Pep Guardiola

Tue, 30 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kwenye soka la kisasa, makocha wengi wanataka wawe na nguvu linapokuja suala la usajili wa mastaa wapya wa kuja kuongeza nguvu kwenye vikosi vyao.

Jambo hilo limeshuhudia makocha wakubwa wa Ulaya kutumia pesa nyingi sana kwenye kunasa mastaa wapya, huku wengine wakifanikiwa kubeba mataji mengi na wengine wakitumia pesa nyingi, mataji kiduchu.

Makocha kama Zinedine Zidane na Sir Alex Ferguson wao hawakutumia pesa nyingi sana kwenye usajili, lakini wamekuwa na mafanikio makubwa ndani ya uwanja, huku Pep Guardiola akifunika wote kwa kufungulia pochi lake na kupata mafanikio makubwa.

Guardiola amesajili mastaa wapya 79, Jose Mourinho mastaa 119, Carlo Ancelotti wakali 109, Massimiliano Allegri wachezaji 114, Diego Simeone (840), Thomas Tuchel (73), Manuel Pellegrini (98), Antonio Conte (93), Mauricio Pochettino (57), Jurgen Klopp (850, Unai Emery (87), Arsene Wenger (104), Jorge Jesus (139), Claudio Ranieri (129), Rafael Benitez (115).

Kwa mujibu wa Transfermarkt hii hapa orodha ya makocha waliotumia pesa nyingi kwenye usajili na idadi ya mataji waliobeba.

10. Jurgen Klopp

Usajili; Pauni 965 milioni

Amebeba: Mataji 12

Jurgen Klopp anatajwa kama mmoja wa makocha bora kabisa waliopata kutokea kwenye kikosi cha Liverpool baada ya kuirudisha timu hiyo kwenye ramani ya mataji ya ligi ya ndani baada ya kusubiri kwa muda mrefu. Hata hivyo, kufikia mafanikio hayo, Klopp amekuwa mtu wa kusajili sana, akinasa sura mpya 85 na kutumia Pauni 965 milioni.

Usajili wake wa pesa nyingi;

1. Darwin Nunez – Liverpool, Pauni 85milioni

2. Virgil van Dijk – Liverpool, Pauni 75milioni

3. Alisson Becker – Liverpool, Pauni 66.8milioni

4. Dominik Szoboszlai – Liverpool, Pauni 60milioni

5. Naby Keita – Liverpool, Pauni 52.75milioni

9. Mauricio Pochettino

Usajili. Pauni 980 milioni

Amebeba: Mataji 3

Akiwa amebeba mataji matatu katika maisha yake ya ukocha, Mauricio Pochettino wa Chelsea atakuwa na kazi kubwa ya kufanyia kazi pesa anazopewa za usajili ili anase wachezaji watakaoleta mataji kwenye timu. Kwenye maisha yake ya soka, Pochettino ametumia Pauni 980 milioni kusajili wapya, ukiwamo usajili wa Moises Caicedo.

Usajili wake wa pesa nyingi;

1. Moises Caicedo – Chelsea, Pauni 115milioni

2. Achraf Hakimi – PSG, Pauni 58milioni

3. Romeo Lavia – Chelsea, Pauni 53milioni

4. Tanguy Ndombele – Tottenham, Pauni 52milioni

5. Christopher Nkunku – Chelsea, Pauni 51milioni

8. Antonio Conte

Usajili; Pauni 1 bilioni

Amebeba: Mataji 9

Antonio Conte kwa sasa yupo zake mapumziko akiponda raha mbali na presha za ukocha baada ya kufutwa kazi huko Tottenham Hotspur. Hata hivyo, kwenye kazi yake ya ukocha, Conte ni miongoni mwa watu waliotumia pesa nyingi kwenye usajili wa wakali wake, akisajili mastaa 93 na kutumia kiasi cha Pauni 1 bilioni. Si mchezo.

Usajili wake wa pesa nyingi;

1. Romelu Lukaku – Inter Milan, Pauni 63.2milioni

2. Alvaro Morata – Chelsea, Pauni 56.4milioni

3. Richarlison – Tottenham, Pauni 50milioni

4. Cristian Romero – Tottenham, Pauni 42.7milioni

5. Achraf Hakimi – Inter Milan, Pauni 36.7milioni

7. Manuel Pellegrini

Usajili: Pauni 1.02 bilioni

Amebeba: Mataji 7

Kocha huyo wa zamani wa Manchester City alikuwa kwenye kikosi hicho cha Etihad wakati kinaanza kwa kasi zama zao za kubeba mataji na kutawala kwenye soka la England. Kwenye maisha yake ya soka, kocha Manuel Pellegrini, aliyewahi pia kuinoa Real Madrid amefanya usajili wa nyota wengi na kutumia Pauni 1.02 bilioni kunasa nyota 96.

Usajili wake wa pesa nyingi;

1. Cristiano Ronaldo – Real Madrid, Pauni 84.6milioni

2. Kevin De Bruyne – Man City, Pauni 65milioni

3. Kaka – Real Madrid, Pauni 57.2milioni

4. Raheem Sterling – Man City, Pauni 54.4milioni

5. Sebastian Haller – West Ham, Pauni 42.3milioni

6. Thomas Tuchel

Amesajili: Pauni 1.02 bilioni

Amebeba: Mataji 13

Kwa sasa anainoa Bayern Munich, Thomas Tuchel alitua Chelsea kwa kishindo na kufanikiwa kunyakua taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na timu hiyo aliyojiunga nayo akitokea Paris Saint-Germain. Kwenye maisha ya ukocha, Tuchel ametumia pesa nyingi sana kwenye usajili, Pauni 1.02 bilioni kunasa mastaa wapya kuongeza ubora timu yake.

Usajili wake wa pesa nyingi;

1. Kylian Mbappe – PSG, Pauni 153milioni

2. Romelu Lukaku – Chelsea, Pauni 96.5milioni

3. Harry Kane – Bayern Munich, Pauni 82milioni

4. Welsey Fofana – Chelsea, Pauni 68milioni

5. Marc Cucurella – Chelsea, Pauni 55milioni

5. Diego Simeone

Usajili: Pauni 1.05 bilioni

Amebeba: Mataji 10

Kwa sasa yupo zake Atletico Madrid mahali ambako analipwa pesa nyingi kutokana na kazi yake ya ukocha. Diego Simeone amefanya mambo makubwa kwenye kikosi hicho, akibeba mataji 10, huku akifungua pochi kisasa kusajili mastaa wapya, akiwa ametumia Pauni 1.05 bilioni. Anazitesa Real Madrid na Barcelona kwenye La Liga.

Usajili wake wa pesa nyingi;

1. Joao Felix – Atletico, Pauni 108milioni

2. Thomas Lemar – Atletico, Pauni 61milioni

3. Diego Costa – Atletico, Pauni 51milioni

4. Vitolo – Atletico, Pauni 30.4milioni

5. Jackson Martinez – Atletico, Pauni 30milioni

4. Massimiliano Allegri

Amesajili: Pauni 1.21 bilioni

Amebeba: Mataji 14

Licha ya kuwa mapumziko kwa miaka miwili kati ya 2019 na 2021, Massimiliano Allegri amekuwa kocha wa Juventus tangu mwaka 2014 na hakika kwenye kikosi hicho, alifanya matumizi makubwa kwenye usajili wa nyota wapya, ambapo alisajili mastaa 113 na kutumia kiasi cha Pauni 1.21 bilioni kwenye kukamilisha dili hizo za mastaa wapya.

Usajili wake wa pesa nyingi;

1. Cristiano Ronaldo – Juventus, Pauni 100milioni

2. Gonzalo Higuain – Juventus, Pauni 76milioni

3. Dusan Vlahovic – Juventus, Pauni 71milioni

4. Bremer – Juventus, Pauni 37.6milioni

5. Federico Chiesa – Juventus, Pauni 37.2milioni

3. Carlo Ancelotti

Amesajili: Pauni 1.47 bilioni

Amebeba: Mataji 26

Maarufu kwa jina la ‘Don Carlo’, kutokana na umahiri wake kwenye soka la kutumia pesa kwenye usajili wa mastaa wapya. Mtaliano huyo anashika nafasi kwenye orodha ya makocha waliotumia pesa nyingi kusajili, Pauni 1.47 bilioni huku akipita kwenye timu za maana kama Chelsea, AC Milan, Bayern Munich, Real Madrid na PSG na Everton.

Usajili wake wa pesa nyingi;

1. Jude Bellingham – Real Madrid, Pauni 88.5milioni

2. Gareth Bale – Real Madrid, Pauni 85.1milioni

3. Aurelien Tchouameni – Real Madrid, Pauni 68.3milioni

4. James Rodriguez – Real Madrid, Pauni 64milioni

5. Fernando Torres – Chelsea, Pauni 50milioni

2. Jose Mourinho

Amesejili: Pauni 1.58 bilioni

Amebeba: Mataji 26

Jose Mourinho amekuwa kocha kwenye klabu nyingi sana kubwa za Ulaya, akipita Chelsea, Real Madrid, Manchester United na Inter Milan kwa kuzitaja kwa uchache. Mreno huyo amezinoa pia FC Porto na Tottenham Hotspur. Katika maisha yake ya ukocha, Mourinho ametumia Pauni 1.58 bilioni kusajili mastaa 118 na kunyakua mataji 26.

Usajili wake wa pesa nyingi;

1. Paul Pogba – Man United, Pauni 89milioni

2. Romelu Lukaku – Man United, Pauni 72milioni

3. Fred – Man United, Pauni 50milioni

4. Nemanja Matic – Man United, Pauni 38milioni

5. Andriy Shevchenko – Chelsea, Pauni 31 milioni

1. Pep Guardiola

Amesajili: Pauni 1.709 bilioni

Amebeba: Mataji 37

Kwenye orodha hiyo, kocha anayeshika namba moja kwa kutumia pesa nyingi kwenye usajili ni Pep Guardiola, kwa majumuisho ya mkwanja wote aliotumia kwenye klabu za Barcelona, Bayern Munich na sasa Manchester City. Guardiola ametumia Pauni 1.709 bilioni na kufanikiwa kubeba mataji 37 ya michuano tofauti.

Usajili wake wa pesa nyingi;

1. Jack Grealish – Man City, Pauni 100milioni

2. Josko Gvardiol – Man City, Pauni 77milioni

3. Ruben Dias – Man City, Pauni 61.2milioni

4. Rodri – Man City, Puani 59.8milioni

5. Zlatan Ibrahimovic – Barcelona, Pauni 59.4milioni

Makocha wengine

Kwenye orodha ya makocha waliotumia pesa nyingi kwenye usajili wa mastaa wapya kwenye timu zao, yumo pia Rafael Benitez, aliyetumia Pauni 782 milioni kusajili wachezaji 115 na kubeba mataji 13, Claudio Ranieri Pauni 782 milioni na kubeba mataji manane, wakati Jorge Jesus amesajili kwa Pauni 805 milioni na kubeba mataji 18, Arsene Wenger usajili wa Pauni 831.9 milioni na kubeba mataji 21, huku Unai Emery akitumia Pauni 888 milioni kwenye usajili na kubeba mataji 11.

Chanzo: Mwanaspoti