Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Si mchezo 2022-2023 ilikuwa kibabe zaidi

Simba 6 Vs Polisi TZ 1 Si mchezo 2022-2023 ilikuwa kibabe zaidi

Mon, 12 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya sarakasi za muda mrefu hatimaye msimu wa 2022/2023 wa Ligi Kuu Bara unafikia tamati Juni 9 mwaka huu huku kila timu ikivuna ilichopanda kufuatia safari ndefu ambayo iliambatana na milima na mabonde mengi.

Wakati ikiwa imesalia michezo miwili tu tayari bingwa ameshapatikana ambaye ni Yanga iliyolitetea taji lake ililolichukua kwa msimu uliopita huku Maafande wa Ruvu Shooting ikiwa ndio timu pekee hadi sasa iliyoshuka daraja.

Katika msimu huu ambao ulikuwa ni wa kusisimua yapo mengi yaliyojiri kama ambayo Mwanaspoti linavyokuletea uhondo mzima.

HAT-TRICK NANE

Msimu huu umekuwa wa moto zaidi kwenye suala la mastaa mbalimbali kufunga mabao matatu (hat trick) kwani licha ya michezo miwili kusalia ila zimefungwa saba tofauti na msimu uliopita ambapo zilifungwa tatu tu.

Nyota wa kwanza kufunga 'hat-trick' msimu huu ni Fiston Mayele wa Yanga katika mchezo dhidi ya Singida Big Stars uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Novemba 17, mwaka jana ambapo timu hiyo ilishinda mabao 4-1.

Nahodha wa Simba John Bocco naye akafuata mfululizo akianza katika ushindi wa mabao 4-0 na Ruvu Shooting Novemba 19 kisha akafunga nyingine dhidi ya Tanzania Prisons kwenye ushindi wa 7-1, Desemba 30 mwaka jana.

Katika mchezo huo nyota mwingine aliyefunga mabao matatu ni Saidi Ntibazonkiza 'Saido' huku Jean Baleke akifunga pia wakati wa ushindi wa mabao 3-0 na Mtibwa Sugar katika mchezo uliopigwa Machi 11, mwaka huu.

Ibrahim Ali 'Mkoko' wa Namungo ameingia kwenye vitabu vya nyota waliofunga 'Hat-Trick' msimu huu wakati wa ushindi wa 3-1 na KMC, katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Januari 24, mwaka huu.

Nyota aliyehitimisha 'Hat-Trick' ya saba ni Stephane Aziz KI wa Yanga wakati kikosi hicho kikishinda mabao 5-0 dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo mkali uliochezwa Aprili 11, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex.

PENALTI 49

Hadi kufikia mzunguko wa 28 penalti 49 zimepatikana ikiwa ni tofauti ya moja tu na msimu uliopita ambao zilikuwa 50.

Katika penalti hizo 49 ni 32 zilizoingia kambani wakati 17 zikikoswa huku Dodoma Jiji ikiwa timu kinara kwa nyota wake kukosa kwa sababu katika sita ambazo ilipata ilifunga moja tu huku zote tano zilizobakia ikikosa.

KADI NYEKUNDU 29

Msimu huu tayari zimetoka kadi nyekundu 29 ikiwa ni zaidi na ilivyokuwa msimu uliopita ambapo zilitoka jumla 24 tu.

Timu inayoongoza kupata kadi hizo ni Polisi Tanzania ambao mastaa wake watano wameshapata huku beki wake wa kati, Mohamed Mmanga akishikilia rekodi ya mchezaji pekee hadi sasa aliyepata kadi nyekundu mbili msimu huu.

Mmanga alipata kadi hizo wakati wa mchezo wa kwanza tu wa ufunguzi wa msimu dhidi ya Yanga Agosti 16, mwaka jana wakati timu hiyo ilipofungwa mabao 2-1 na ule wa Ruvu Shooting Septemba 19, mwaka jana waliofungwa bao 1-0.

WALIOJIFUNGA 18

Msimu uliopita mastaa 20 walijifunga ila hadi sasa ikiwa imesalia michezo miwili Ligi Kuu Bara kutamatika ni nyota 18 tu waliojifunga wakati Dodoma Jiji na Geita Gold wachezaji wake wakiongoza mara tatu kwa kila timu.

MAYELE, SAIDO WATEKA SHOO

Nyota wa Yanga, Fiston Mayele amefikia rekodi ya mabao aliyoiweka msimu uliopita ya kufunga 16 katika Ligi Kuu Bara akihitaji bao moja tu kuifikia ya aliyekuwa mshambuliaji wa Geita Gold, George Mpole aliyefunga 17.

Mpole alifunga mabao hayo msimu uliopita na kuweza kutwaa kiatu cha ufungaji bora hali iliyozivutia timu mbalimbali kuhitaji saini yake ila ilikuwa ni FC Lupopo ya DR Congo iliyomnasa dirisha dogo la Januari mwaka huu.

Wakati Mayele akiendelea kuongoza kwa ufungaji bora nyota wa Simba Mrundi, Saidi Ntibazonkiza 'Saido' ndiye mchezaji anayeongoza katika michezo ya Ligi Kuu Bara msimu huu kuhusika kwenye mabao mengi zaidi ya wengine.

Saido aliyeanza msimu huu na Geita Gold baada ya kuachana na Yanga Mei 30, mwaka jana amekuwa kwenye kiwango kizuri tangu ajiunge na Simba dirisha dogo la Januari mwaka huu licha ya baadhi yao kuubeza usajili wake.

Kabla ya mechi za jana Saido alikuwa amefunga mabao 15, yakiwamo 11 akiwa na Simba na mengine manne aliyotupia alipokuwa Geita, huku akiasisti 12 zikiwamo sita za Geita na zilizobaki akiwa na kikosi cha Simba (kumbuka jana alikuwa tena uwanjani kukabilianan na Coastal Union).

Ubora wa Saido umemfanya nyota huyo kuivunja rekodi yake aliyoiweka msimu uliopita wakati akiichezea Yanga kwani katika michezo 18 aliyocheza alihusika kwenye mabao 10 ambapo alifunga saba na kuchangia matatu tu.

WAZAWA WANG'ARA

Kabla ya jana wakati ligi ikifikia tamati yalikuwa yamefungwa mabao 537 yakiwamo 48 yaliyotokana na penalti, huku wazawa wakifunika kwa kufunga 331 kupitia wachezaji 135, ilihali nyota wa kigeni 55 wakifunga jumla ya mabao 191. Mabao mengine 18 ya ligi hiyo yalikuwa ni ya kujifunga.

Hata hivyo idadi ilitarajiwa kuongezeka kwa nyota wote wa pande mbili sambamba na hata penalti kutokana na ukweli jana kulikuwa na mechi nane zinapigwa viwanja tofauti, ambayo yangeweza kubadilisha namba za mabao, kadi, penalti na hata kujifunga kwa wachezaji wakati wakifunga msimu.

MSIKIE PLUIJM

Akizungumzia msimu jinsi ulivyokuwa Kocha Mkuu wa Singida Big Stars, Hans Van Der Pluijm anasema ushindani ulikuwa mkali kutokana na maandalizi ya kila timu hivyo anategemea hali hiyo itaendelea zaidi msimu ujao.

"Ni msimu wa kwanza kwetu Ligi Kuu Bara ila tumeona jinsi ugumu ulivyokuwa kwani hii inaonyesha dhahiri kama huna kikosi bora na kipana huwezi kutimiza malengo uliyojiwekea hivyo nategemea ushindani zaidi msimu ujao."

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: