Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Si Mbape wala Bellingham kusajiliwa Man United

Mbape  Bellingham Si Mbape wala Bellingham kusajiliwa Man United

Thu, 21 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kama wewe ni shabiki wa Manchester United na una ndoto za kumwona supastaa Kylian Mbappe kikosini Old Trafford, amka usingizi, usiendelee kuota hiyo njozi. Unajua kwa nini? Mwenye pesa za kumleta Mfaransa huyo aje kucheza Old Trafford, amesema hana huo mpango.

Iko hivi, bilionea mpya wa Man United, Sir Jim Ratcliffe, ambaye ndiye mwenye majukumu ya kusimamia mambo yote ya maendeleo ya soka kwenye timu hiyo, ameweka kando mpango wa kumsajili Mbappe kwenye dirisha lijalo.

Si Mbappe pekee, bali tajiri huyo wa Uingereza amemfuta pia kwenye mipango yake, kiungo wa Real Madrid, Jude Bellingham kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya.

Bilionea, Ratcliffe, 71, anamiliki hisa asilimia 25 za klabu ya Man United kwa gharama za Pauni 1 bilioni kutoka kwa wamiliki wakuu wa timu hiyo, familia ya Glazer baada ya mashabiki kuangamana.

Bosi huyo wa INEOS anajaribu kuleta mtazamo mpya kwenye kikosi hicho, akitaka waondokane kwenye mfumo wa kizamani ambao umeshindwa kuleta mafanikio kwenye timu tangu Sir Alex Ferguson alipoondoka kwenye kikosi hicho.

Akizungumza na Geraint Thomas ambaye anasimamia michezo ya baiskeli kwenye kampuni ya INEOS, Ratcliffe alifuta wazo la kuwasajili Mbappe na Bellingham katika kipindi cha miaka michache ijayo.

“Ni mwanasoka mahiri, lakini hayupo kwenye mipango yetu,” alisema Ratcliffe alipoulizwa kama ana mpango wa kumleta Bellingham uwanjani Old Trafford. “Suluhisho sio kutumia pesa nyingi kwa wachezaji mahiri. Tumefanya hivyo mara nyingi kwenye kipindi cha miaka 10 iliyopita.

“Kitu cha kwanza tunachotaka kufanya ni kuleta watu sahihi, wataongoza klabu. Lazima tuhakikishe tunafanya usajili sahihi, hicho ndicho kitu muhimu kwenye mchezo wa soka, kufanya usajili sahihi wa wachezaji wapya.”

Man United imetumia zaidi ya Pauni 1 bilioni tangu Ferguson alipoondoka, lakini imeshindwa kabisa kuongeza idadi yao ya mataji na kukwama kwenye mataji yaleyale 13 ya Ligi Kuu England waliyobeba wakiwa na kocha huyo raia wa Scotland.

Ratcliffe alipoulizwa kuhusu Mbappe, alisema: “Ni heri nimtafute Mbappe mpya, kuliko kutumia pesa nyingi kununua mafanikio. Sio ujanja kumnunua Mbappe.”

Baada ya misimu mitano ya mafanikio makubwa kwenye Ligue 1 akiwa na kikosi cha Les Parisiens alikojiunga akitokea Monaco mwaka 2017, Mbappe anatarajia kwenda kujiunga na Real Madrid inayoshiriki mikikimikiki ya La Liga.

Licha ya kubeba mataji ya kutosha Parc des Princes, Mbappe mwenye umri wa miaka 25, ameshindwa kuipa timu hiyo ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na kwa msimu huu kikosi hicho kipo chini ya kocha Luis Enrique na kimetinga hatua ya robo fainali na itakipiga na Barcelona mwezi ujao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live