Baada ya matokeo ya Jumapili iliyopita ya Yanga kupoteza nyumbani dhidi ya USM Alger ni rahisi kutabiri kwamba wamekosa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika. Matokeo hayo yanamaanisha Yanga itahitaji kushinda walau mabao 2-0 ugenini ili itwae ubingwa. Matokeo ambayo haionekani kwa namna ambavyo USM Alger imecheza kwa Mkapa.
Vinginevyo ni Yanga kushinda mabao 2-1 kisha kuupeleka mchezo katika hatua ya matuta. Ni kwa jinsi gani Yanga itapata mabao mawili ugenini kama imeshindwa kwa Mkapa? Hatuna majibu.
Mojawapo kati ya vitu bora zaidi kwa Yanga msimu huu ni uwezo wa kupata bao ugenini. Wamefunga bao wakiwa nchini Nigeria, DRC, Tunisia na hata Afrika Kusini. Mara chache Yanga wamewahi kuwa na mwendelezo huu ugenini.
Unapokuwa na timu ya namna hiyo ni vyema kuweka akiba ya maneno. Unapokuwa na mshambuliaji kama Fiston Mayele muda wowote unaweza kupata bao. Mabao yake saba kwenye michuano hii yanaonyesha ubora wake mbele ya lango.
Je, bado na wewe unaamini kuwa kuna muujiza kule nchini Algeria unaokwenda kutokea? Niandikie ujumbe mfupi wa maoni yako kupitia namba yangu ya simu hapo juu.
Nafikiri Yanga wanaweza kwenda ugenini na kujaribu kuondoka na muujiza, lakini itahitaji zaidi Mungu awe upande wake kuliko mipango yao. USM Alger watakuwa hatari zaidi mbele ya mashabiki wao na watawaweka Yanga matatani zaidi.
Yanga watashambuliwa tofauti na wanavyofikiri. Bado fainali ni mafanikio kwa Yanga na hawapaswi kuumia kama watapoteza kombe. Tangu mwanzo kutwaa taji haukuwa mpango wao.
Kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika haukuwa mpango wa Yanga wala shabiki yeyote wa soka hapa nchini. Hakuna chochote unaweza kuwadai Yanga. Wamepambana sana. Wameupiga mwingi bahati mbaya mchezo wa soka unahitaji makombe kupewa heshima.
Lakini kwa hapa walipofika Yanga hata kama hawatapata kombe kuna namna unapaswa kuwaheshimu. Yanga ndiyo Manchester City ya ukanda wetu wa Cecafa. Yanga ndiyo fahari ya Afrika Mashabiki. Mechi ya Uwanja wa Mkapa ilikuwa kubwa sana kiakili kwa Yanga.
Ni mechi ambayo hisia zilikuwa juu kwa wachezaji, benchi la ufundi mpaka mashabiki wenyewe. USM Alger ni kama walikuwa uwanja wa nyumbani.
Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi ni bingwa haswa wa mbinu. Ni fundi wa kuusoma mchezo na kufanya mabadiliko, lakini nadhani kuna kitu hakipo sawa kwenye ufundi wake.
Sina lengo la kumkosea heshima, lakini nadhani Tuisila Kisinda na Aziz KI hakuna kati yao anayetakiwa kumuweka benchi Bernard Morrison. Morrison anaweza kuwa na matatizo mengi nje ya uwanja, lakini ndani ni bora kuliko wote niliowataja.
Bado sielewi kwa nini anawekwa benchi kwenye mechi muhimu kama hizi. Mechi inaonekana ilikuwa ngumu kwenye vichwa vya wachezaji kuliko hata uwanjani. Changamoto pia ya uwanja kutokana na mvua kuna namna ilipunguza ladha halisi ya mpira.
Nilidhani Yanga walipaswa kucheza mipira mirefu ili kukwepa mtego wa uwanja. Nilidhani Yanga watapiga mipira mirefu ili wanufaike na mbio za Mayele, Musonda na Kisinda. Matokeo yake bado walicheza pasi zao fupi kama kawaida, wakalala kwa mbao 2-1.
Unawaona Yanga wakifanya muujiza nchini Algeria na kurudi na Kombe? Naomba maoni yako kupitia ujumbe mfupi wa maandishi kwa namba ya simu hapo juu.
Mara ya mwisho Yanga na USM Alger pale nchini Algeria walikutana 2018. Yanga ilifungwa mabao 4-0. Sio kumbukumbu nzuri kwa Wananchi. Sio rekodi inayotia moyo.
Kocha wa Yanga anahitaji kwenda kujilipua. Yanga wanahitaji kwenda kupambana kiume wana wachezaji wenye uwezo wa kulazimisha matokeo mazuri ugenini.
Kwenye mchezo wa soka ukishakuwa na timu yenye uwezo wa kufunga bao uko salama uwanja wowote. Yanga wana Mayele na Musonda hakuna lisilowezekana.
Nadhani kuna haja ya kuangalia mbadala wa Aziz KI na Kisinda kwenye kikosi cha kwanza. Kuna haja ya Morrison, Jesus Moloko au Farid Mussa kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza. Kuna haja ya kutafuta kiungo mbunifu kama Aboubakari Salum 'Sure Boy' kwenye mechi ya marudiano.
Mtihani ni mgumu kwa Yanga, lakini kwenye soka kila kitu kinawezekana. Kila mtu ana namna anavyotazama mechi. Kila mtu ana maoni yake kama kuna namna unadhani Yanga wanaweza kupindua matokeo ugenini tafadhali usisite kuniandikia ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo juu. Mechi ya marudiano ni ngumu zaidi kwa Yanga lakini naamini bado wana nafasi ya kutwaa ubingwa.