Bonge la shoo. Hapana ni bonge la mechi. Ndicho mashabiki wanachowaza kitakachokwenda kutokea Wembley leo hii Jumamosi, huku wengine wakisema atakayepigwa apigwe tu.
Ni hivi, Manchester City na Manchester United zitakipiga katika kipute cha fainali ya Kombe la FA, ikiwa ni Manchester derby ya tatu kwa msimu huu - huku mbili zilizopita kila mtu alishinda kwake.
Man City ya Pep Guardiola, yenyewe inafukuzia rekodi ya kihistoria ya kubeba mataji matatu makubwa ndani ya msimu mmoja, ili iifikie Man United ilipofanya hivyo chini ya Sir Alex Ferguson mwaka 1999.
Tayari wameshabeba taji la Ligi Kuu England, na wakimalizana na Man United kwenye fainali ya Kombe la FA, watakuwa na fainali nyingine ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Inter Milan itakayopigwa Istanbul wiki ijayo.
Kwa upande wa kocha Erik ten Hag na chama lake la Man United, atakuwa na nafasi ya kubeba taji lake la pili katika msimu wake wa kwanza kwenye kikosi hicho baada ya kubeba Kombe la Ligi, huku timu ikimaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England na kukamatia tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Siku zote, Manchester derby imekuwa na upinzani mkali ndani na nje ya uwanja, ambapo mashabiki wa kila timu watahitaji ushindi ili kuwatambia wenzao. Man United watamaliza msimu wao leo, wakati Man City wao watasubiri kumaliza na Inter Milan huko Istanbul. Lakini, kwa sasa akili na mipango ya timu zote imeelezwa Wembley.
Wamefikaje fainali?
Man United imekamatia tiketi ya kucheza fainali ya Kombe la FA msimu huu baada ya kuwachapa Brighton kwa mikwaju ya penalti. Baada ya sare ya bila kufunga katika dakika 120, mikwaju ya penalti ilifuata na hapo Man United ikakamatia tiketi ya kwenda kucheza fainali na Man City, ambao wao kwenye nusu fainali walicheza na Sheffield United na kuwachapa 3-0, shukrani kwa mabao ya Riyad Mahrez, aliyefunga hat-trick siku hiyo.
Mtihani unaowakabili Man United ni kuhakikisha wanawazuia mahasimu wao hao wasijiweke kwenye wakati mzuri wa kubeba mataji matatu msimu huu ili kulinda rekodi yao ya kihistoria.
Ubora wao upoje?
Man City: Ilichapwa 1-0 katika mechi yao ya mwisho ya Ligi Kuu England ilipokipiga na Brentford, lakini ilikuwa haijapanga kikosi chake cha nguvu kwa kuwa tayari ilishakuwa imebeba ubingwa. Kabla ya mechi hiyo, ilitoka sare ya 1-1 na Brighton - mechi ambayo pia tayari ubingwa ulikuwa kwenye begi.
Lakini, ubora halisi wa Man City ilikuwa kwenye mechi ilizocheza kupata kitu, kwenye ule ushindi wa 1-0 dhidi ya Chelsea na ule wa 4-0 dhidi ya Real Madrid kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Wanapokuwa kwenye ubora wao, Man City haizuiliki.
Man United: Imekuwa na ubora wa kupanda na kushuka, kuna wakati wamekuwa tishio sana, lakini kuna nyakati nyingine utashangaa wanachofanya uwanjani, kama vile ilivyotokea kwenye mechi ya kipigo cha mabao 7-0 kutoka kwa Liverpool. Lakini, wamemaliza namba tatu kwenye ligi na hayo ni mafanikio makubwa kwa Ten Hag. Kingine, Man United imeshinda mechi zake zote nne za mwisho, ikiwamo ushindi wa 4-1 dhidi ya Chelsea.
Taarifa za vikosi vikoje?
Man City: Guardiola ana wasiwasi juu ya afya za mastaa wake watano, akiwamo Kevin de Bruyne, Jack Grealish na Ruben Dias. Mastaa hao si majeruhi wa kutisha, lakini huenda akafikiria kuwatumia zaidi kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kuliko fainali hii ya Kombe la FA.
Man United: Ten Hag hatakuwa na saini ya Anthony Martial na Antony baada ya wawili hao kuwa majeruhi. Jadon Sancho anatazamiwa kuanza kwenye ile safu ya wakali watatu wa mbele, sambamba na Marcus Rashford na mmoja kati ya Alejandro Garnacho au Wout Weghorst. Mastaa wakuchungwa katika fainali hiyo, kwa Man United ni Rashford na Man City ni Erling Haaland.
Rekodi za mechi zao
Rekodi za mechi zote, Man United na Man City zimekutana mara 165 - ambapo Man United imeshinda 65, Man City 52 huku sare zikiwa 48. Kombe la FA zimewahi kukutana mara mbili, kila mmoja akishinda moja wakati kwenye Kombe la Ligi zimekutana mara sita na kila upande ukishinda mara tatu.
Kwenye Ligi Kuu England zimekutana mara 156, Man United imeshinda 60 na Man City 48, huku kukiwa na mechi 48 zilizomalizika kwa sare. Ngao ya Jamii zimekutana mara moja tu na Man United ilishinda mechi hiyo. Mechi zao zilizalisha mabao 464, Man United imefunga 230 na Man City 234. Safari hii atapigwa nani? Ngoja tuone kipute cha kikubwa.