By Clezencia TryphoneMore by this AuthorBy Charles AbelMore by this Author UKISIKIA shoo shoo ndio leo wakati michuano ya Simba Super Cup, ikifikia kilele kwa wenyeji Simba kumalizana na Tp Mazembe ya DR Congo, huku Kocha Mkuu, Didier Gomes akisisitiza hakuna anachokitaka zaidi ya ushindi na shoo tamu itakayowaburudisha mashabiki wao uwanjani.
Huu ni mchezo wa pili kwa Gomes akiwa na kikosi cha Simba na katika mchezo wao dhidi ya Al Hilal, Wekundu hao waliupiga mwingi na kuwapa burudani mashabiki, kitu ambacho Mfaransa huyo amesisitiza kwa leo itakuwa mara mbili kwani amepata muda zaidi wa kuwapa madini vijana wake.
Simba inayoongoza msimamo wa michuano hiyo maalumu iliyoasisiwa kwa ajili ya kuipa maandalizi ya mechi zao za makundi zitakazoanza kupigwa kuanzia Februari 12, ikiwa na alama tatu sawa na Al Hilal, lakini wakibebwa na uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa. Simba imepangwa Kundi A katika Ligi ya Mabingwa na Al Ahly ya Misri, AS Vita ya DR Congo na El Merreikh ya Sudan.
Mechi ya leo inaipa nafasi kubwa Simba kumaliza kibabe michuano hiyo mbele ya Mazembe waliopoteza 2-1 juzi mbele ya Al Hilal kutoka Sudan, katika mchezo wao utakaopigwa kuanzia saa 11:00 jioni na utakaosindikizwa na burudani tamu kutoka kwa mwanadada mkali Zuchu wa WCB, huku Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa ndiye atakayekuwa mgeni rasmi wa kilele cha michuano hiyo iliyoshirikisha timu tatu.
Ushindi au sare ya aina yoyote katika mchezo wa leo ni matokeo yatakayoifanya Simba ijihakikishie ubingwa wa michuano hiyo na kubakisha kitita cha Sh15 milioni kilichotengwa kwa bingwa wa msimu huu wa kwanza sambamba na kombe na medali za dhahabu za mshindi wa kwanza.