Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shime aipigia hesabu robo fainali Kombe la Dunia

Serengeti Girls Robo Timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Girls’

Tue, 18 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Ushindi wa mabao 2-1 ilioupata Timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Girls’ dhidi ya Ufaransa umeamsha ari ya timu hiyo kutinga hatua ya robo fainali za fainali hizo za Kombe la Dunia zinazoendelea nchini India.

Mabao ya Serengeti yaliwekwa nyavuni na Diana Mnally dakika ya 16 na Christer Bahera dakika ya 56 kwa penalti, wakati lile la Ufaransa lilifungwa na Lucie Calba dakika ya 75.

Huo ni ushindi wa kwanza kwa timu hiyo iliyopo Kundi D kwenye fainali hizo kufuatia mechi iliyopita kufungwa mabao 4-0 na mabingwa wa kombe hilo 2014 Japan ambao wanashiriki kwa mara ya saba.

Akizungumza kocha mkuu wa timu hiyo, Bakari Shime alisema ushindi umeamsha morali katika kikosi chake hivyo imani yake ni kutinga hatua ya robo fainali ingawa haitakuwa kazi rahisi.

“Matokeo haya yametupa mwanga na jinsi ya kujipanga zaidi kwenye mechi yetu inayofuata, tunacheza na timu zilizo bora ila nasi tuna kikosi cha kupambana,” alisema na kuongeza;

“Jambo kubwa tunalolizingatia ni kucheza kwa tahadhari na kwa malengo kwa sababu mchezo umebaki mmoja wa kuamua hatima yetu kwenye mashindano haya makubwa duniani.”

Kikosi hicho kinashuka uwanjani kesho Jumanne kumenyana na Canada katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi kwenye Uwanja wa DY Patil ambao upo Mji wa Navi, huko nchini Mumbai India.

Tangu michuano hii imeanzishwa mwaka 2008, Canada imeshiriki katika kila msimu ambapo huu ni wa saba kwake na mara yao ya mwisho kushiriki ilikuwa mwaka 2018 ilipomaliza katika nafasi ya nne.

Katika kundi hilo Japan ndiye anayeongoza kwa kukusanya pointi sita huku Serengeti ikiwa ya pili na pointi tatu wakati Ufaransa, Canada zipo ya tatu na nne zikiwa na pointi moja kila timu.

Washindi wawili kutoka kwenye kila kundi watafuzu moja kwa moja hatua ya robo fainali ya michuano hii.

Chanzo: Mwanaspoti