Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shikangwa: Straika Simba Queens anayeiwaza England

Jentrix Shikangwa Straika wa Simba Queens, Mkenya Jentrix Shikangwa

Thu, 4 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Makipa wa Ligi Kuu ya wanawake wanamfahamu vizuri straika wa Simba Queens, Mkenya Jentrix Shikangwa ambaye alikuwa mfungaji bora wa WPL msimu uliopita akifunga mabao 19.

Baada ya kufanya vizuri msimu huo, Simba ilimuuza kwenda Beijing ya China kwa mkataba wa miezi sita na mkataba wake ulipoisha akarejea tena msimu huu.

Fundi huyo wa kufumania nyavu tayari kaweka nyavuni mabao manne msimu huu kwenye mechi mbili na kutoa asisti tatu za mabao, wastani wa kufunga mabao mawili kila mechi.

Mwanaspoti lilimtafuta straika huyo na kufanya mahojiano naye kuanzia safari yake ya soka hadi kufika Simba Queens.

ALIPOANZIA Anasema alianza kucheza soka akiwa darasa la sita katika Shule ya Shipalo, Kenya mwaka 2013 na kuendelea hadi sekondari kuichezea timu ya shule ya Wiyeta.

“Baada ya kucheza sana shule, Vihiga Queens waliniona na nikaanza kucheza na hapo nikapata timu ya nje ya Fatih Karagumkur ya Uturuki na kucheza kwa miezi sita ndio msimu wa 2022 nikajiunga na Simba nikasaini mwaka mmoja kisha nikajiunga na Beijing ya China na msimu huu nimerudi Simba hiyo ndio historia yangu,” anasema Shikangwa.

ANAIOTA ENGLAND Tayari amecheza timu tatu nje ya Kenya, Simba Queens, Karagumruk ya Uturuki na Beijing ya China lakini kwenye akili yake anatamani kucheza soka la kulipwa England.

“Ndoto yangu ni kucheza soka England kwani ni ligi yenye ushindani ukizungumzia soka la wanawake kwa Ulaya hivyo itaniongezea kitu kwenye fani yangu ya soka,” anasema Shikangwa.

HAPA ALIINJOI

Anasema hakuna kipindi alifurahia kama mwaka 2019 ambako aliibuka mfungaji bora wa mashindano ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) akiweka kambani mabao 10.

Mwaka huo Kenya iliibuka mabingwa wa CECAFA Challenge na kuitoa Tanzania kwa jumla ya mabao 2-0 yote yakifungwa na Shikangwa.

Hakuishia hapo, msimu wa 2021 akiwa na Vihiga Queens aliibuka mchezaji bora wa michuano ya Ligi ya Mabingwa ya kwa Wanawake.

“Yaani naweza kusema nilikuwa na wakati mzuri zaidi kuisaidia timu yangu ya taifa tulivyokuja hapa Tanzania kwenye mashindano ya CECAFA na kuibuka mfungaji ilikuwa rekodi nyingine kwangu,” anasema Shikangwa.

MANENO HAYA MHH!

Anasema hakuna kitu kinamtoa mchezoni kama kujitoa kwa asilimia zote kuisaidia timu halafu kocha asione umuhimu wake kwenye kikosi.

“Naweza kuvumilia vyote lakini kuna maneno kwenye soka la wanawake yananichukiza kama kocha kutoona umuhimu wangu kikosini, hiyo kitu inaniumiza sana.”

UNESI FRESHI

Mkali huyo wa mabao anasema isingekuwa soka basi angekuwa anawahudumia watu hospitalini kwani ni kitu anachokipenda tangu akiwa mtoto.

“Mpira naupenda sana tangu nikiwa mdogo ndio ndoto yangu kubwa ya kwanza, lakini nisingekuwa mchezaji basi nafikiri ningekuwa nesi kwa kuwa ni kitu kingine nakipenda.”

KIATU CHA DHAHABU

Ukiachana na kufunga kwenye mashindano mbalimbali ya kimataifa na Ligi ya Kenya msimu uliopita wa Ligi ya Wanawake (WPL) ndio alikuwa mfungaji bora akiweka nyavuni mabao 19.

Licha ya timu yake msimu uliopita kuukosa ubingwa lakini alichukua kiatu na kuwaacha wazawa wa JKT Queens, Donisia Minja aliyefunga 17 na Stumai Abdallah 13.

Anasema msimu huu amerudi ligi ikiwa tayari imechezwa mechi saba hivyo atapambana kuhakikisha anafunga mabao zaidi ya msimu uliopita.

“Natamani kufunga mabao 20 kama nitapata nafasi ya kucheza na kufunga japo najua sijaanza msimu nimekuta tayari ligi inaendelea ila naamini nitapambana kuhakikisha sichezei nafasi ninayopewa,” anasema Shikangwa.

ISHU YA ULAYA

Kabla ya kujiunga na Simba mwaka 2023 alifanikiwa kujiunga na timu ya Karagumruk ya Uturuki kwa mkataba wa miezi sita na kukumbana na changamoto nyingi ikiwemo ya kukosa namba.

Anasema kila kocha alikuwa na mchezaji wake hivyo ilikuwa ngumu kupata namba ya kucheza jambo lililomfanya ashindwe kuonyesha kiwango chake na kufanikiwa kufunga mabao sita.

“Nilikumbana na changamoto nyingi sana unaweza kuwa unafanya vizuri lakini kama hawaoni mchango wako na hata unashindwa kupata muda wa kucheza kila anampambania mchezaji wake unashindwa kufosi kuomba kucheza.”

FAMILIA

Kila mwanamke ana ndoto ya kuwa na watoto na familia na kwa Shikangwa anasema kwake anatamani kupata familia akiwa tayari amestaafu soka.

“Natamani nimalize kabisa mihangaiko ya soka ndio nijenge familia na wazazi wangu wamekuwa msaada mkubwa pale nipapokwama wamekuwa wakinisapoti sana.”

Alipoulizwa kuhusu mahusiano alisema “Hilo siwezi kuzungumzia kwenye vyombo vya habari kabisa mengine ni siri.”

HADI KUKABA

Anasema kingine watu wasichojua kumhusu yeye ana uwezo wa kucheza kama beki wa pembeni ‘fullback’ bila wasiwasi na kukaba vizuri tu.

“Mchezaji anatakiwa kuwa anacheza nafasi nyingi, kuna siku mmoja wenu amepata dharura, timu inakuwaje, hivyo mbali na kulijua goli pia naweza kucheza kama ‘fullback’.”

HACHAGUI

Kwake hajawahi kuchagua mlo, chakula chochote yeye twende kazi ili mradi kisiwe na madhara kiafya hasa kwa wachezaji.

“Chakula ninachokipenda sana ni pilau na hakuna chakula ambacho mimi sikipendi isipokuwa huwa tunachukua tahadhari ya baadhi ya vyakula ambavyo tunashauriwa na wataalamu wa afya,” anasema.

Chanzo: Mwanaspoti