Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, amegusia nia yao ya kuweka teknolojia ya usadizi kwa marefa (VAR) kwenye viwanja vyetu.
Kimsingi wazo hilo ni jema kwa sababu katika karne hii ya sayansi na teknolojia vitu kama hivi haviepukiki. Wazo la VAR nchini lilianza msimu wa 2021/22 baada ya mchezo wa Yanga na Mbeya City, Februari 5, 2022, ulioisha kwa sare tasa.
Shabiki mkubwa wa Yanga ambaye alikuwa Waziri wa Fedha (hadi sasa), Mwigulu Nchemba aliandika kwenye ukurasa wake wa X (wakati huo Twitter) kwamba atazungumza na waziri mwenzake mwenye dhamana michezo (wakati ule alikuwa Mohamed Mchengerwa) ili serikali inunue VAR.
Siku chache baadaye waziri huyo mwenye dhamana ya michezo, Mchengerwa ambaye alikuwa mmiliki wa timu ya Rufiji United hapo kabla akasema serikali inafikiria kununua teknolojia hiyo.
Teknolojia hiyo ambayo ni ya gharama kubwa hupunguza uamuzi tata ambao husababishwa na upungufu wa kibinadamu wa waamuzi pamoja na kasi ya mchezo wa kisasa.
Lakini ukiliangalia kwa kina zaidi suala hilo utaona sisi kama taifa ambalo hata kwenye sayansi na teknolojia bado liko nyuma kwa sasa hatuihitaji teknolojia hiyo.
Sisi tunahitaji zaidi viwanja bora kuliko VAR. Mpira wetu unachezwa kwenye viwanja vingi vya hovyo. Viwanja ni vya hovyo kwa kila nyanja kuanzia eneo la kuchezea, vyumba vya kuvalia hadi wanapokaa mashabiki majukwaani.
Badala ya kutumia mabilioni kuinunua teknolojia hiyo ambayo haitamaliza tatizo la uamuzi, ni bora hizo pesa tukazitumia kuwekeza kwenye miundombinu.
VAR ni teknolojia inayotumika sehemu mbalimbali duniani na huko kote kila siku wanailaumu. Kwenye mashindano ya African Football League yaliyomalizika hivi karibuni, klabu ya Al Ahly ya Misri iliandika barua rasmi kwa CAF ikilalamikia uamuzi katika mechi ambazo VAR ilitumika.
Huko Ulaya ndiyo usiseme. Kila siku makocha wanalalamikia VAR na nchi kama England kila wakati mwenyekiti wa kamati ya waamuzi amekuwa akijitokeza kuomba radhi kwa makosa ya VAR.
Sasa kuna haja gani kutumia mabilioni ya fedha kwa ajili ya teknolojia hii ambayo haitatusaidia kwa asilimia 100 kutatua matatizo yetu?
Hayo mabilioni si ni bora yakatumika kutengeneza miundominu.
GHARAMA ZA VAR
Kusimika mtambo wa VAR pekee kunagharimu Pauni 4.6 milioni, sawa na zaidi ya Sh14.5 bilioni za Tanzania.
VAR huendeshwa chini ya Bodi ya Kimataifa ya Mpira wa Miguu (Ifab - International Football Association Board). Hii ina maana kwamba ukihitaji kusimika VAR nchini mwako utalazimika kuipata kutoka kwao tu.
Mwaka 2022, Azam TV walijaribu kutumia kamera zao tu kufanya kama VAR kwenye ligi ya vijana pale Chamazi. Likaja karipio kali kutoka Fia na Ifab kuhusu hilo.
Gharama za uendeshaji zipo juu sana. Hufika hadi Sh30 milioni kwa mechi pamoja na VAT. Kwa ligi yetu yenye michezo 240 itabidi itoke sio chini Sh7 bilioni kwa msimu.
Gharama zote hizo za nini ilhali bado tuna mambo mengi ya kufanya. Kwanini hizi pesa tusitumie kutengeneza vitu ambavyo tutavitumia leo, kesho na keshokutwa?
Kwanini tusijenge vituo vya ufundi kama kile cha Tanga na Kigamboni katika mikoa mingine nchini?
Wenzetu wanaweka VAR baada ya kumaliza mambo yote haya madogo madogo. Viwanja vyao ni bora. Wana vituo bora na kila kitu chao ni bora. Ndiyo maana sasa wanawaza anasa hii.
Leo hii kwa kuwa hatuna VAR tunadhani matatizo ya kina Hery Sasii tutayamaliza kwa VAR.
Hii ni sawa tu na mtoto yatima anayepata tabu, atawaza “angekuwepo baba nisingeteseka namna hii.” Lakini kumbe kuna wenzake wengi wanateseka kama yeye na baba zao wapo.
Hata yeye yawezekana huyo baba yake mwenyewe hakuwa na uwezo wa kuzuia haya mateso anayoyapata, lakini kwa kuwa hayupo basi kila kitu “angekuwepo baba.”
Leo tunaitaja VAR kwa sababu haipo siku ikiwepo na ikatufanyia yaleyale ya England tutaanza kuitukana na kuilaani vibaya. Wakati huo ukifika ndiyo tutaanza kukumbuka kuwa tumepoteza fedha nyingi kugharamia kitu ambacho hakitusaidii.
Hatuhitaji VAR kwa sasa. Tunahitaji miundombinu bora na ya kisasa kwa ajili ya maendeleo ya mchezo wetu pendwa.