Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sheria zetu za CAF, TFF zinaturudisha nyuma

CAF Motsepe.jpeg Mkutano wa Viongozi wa CAF

Fri, 25 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Aendelee kupumzika kwa amani Justin Kalikawe, mwanamuziki wa reggae ya Kiswahili aliyeanza kazi yake miaka ya 1980 akafikia kilele miaka ya 1990 na kufariki dunia 2003.

Moja ya kazi zake ni UTARATIBU WETU, wimbo wa 12 kwenye albamu ya MV Bukoba.

Utaratibu wetu wenyewe unatukandamiza sisi wenyewe. Nimeukumbuka sana wimbo huu baada ya sakata la baadhi ya makocha wa Ligi Kuu Bara kuonekana hawana vigezo vya kufanya majukumu yao.

Hiki ni kitu ambacho hakijaelezewa kwa kina kiasi kwamba watu wengi hawakielewi vizuri. Ili kuweza kulielewa vizur hili sakata inabidi turudi nyuma hadi Mei 2021 pale Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lilipokuja na mabadiliko kwenye vigezo vya makocha wa kufundisha katika mashindano yake ya klabu yaani Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.

Taarifa iliyotolewa na CAF na kusainiwa na naibu katibu mkuu wake, Anthony Baffoe anayeshughilikia maendeleo ya kiufundi ya mpira ilisema matakwa ya leseni za makocha wakuu na wasaidizi kwa mashindano ya klabu ya CAF kuanzia msimu wa 2021/22 ni leseni A ya CAF kwa wakuu na leseni B wasaidizi.

Kwa makocha waliosoma nje ya Afrika kama Ulaya (UEFA), Asia (AFC) na Amerika Kusini (Concacaf) wanatakiwa kuwa na leseni za juu kabisa za Pro Licence kutoka mabara yao - kwa makocha wakuu na leseni A wasaidizi.

Sheria hii ilimaanisha CAF wameyaweka mafunzo yao kwenye daraja la juu zaidi duniani kuliko mafunzo yanayotolewa na bara jingine lolote. TFF ikaichukua sheria hii kama ilivyo na kuileta Tanzania.

Kwa maana hiyo makocha wote wenye leseni A ya Ulaya wakija Afrika, ikiwemo Tanzania Bara wanahesabika kuwa sawa na leseni B. Yaani leseni A ya UEFA kwa Tanzania ni sawa na leseni B...kweli? Yaani Diploma A ya UEFA ni sawa na Diploma B ya Afrika...kituko. Mafunzo ya ukocha husimamiwa na shirikisho la soka la bara na kuendeshwa na vyama vya soka vya nchi wanachama. CAF kama Shirikisho la Soka Afrika husimamia mafunzo barani na TFF kama Shirikisho la Soka Tanzania huendesha mafunzo hapa nchini.

Yaani ukienda pale Karume au Myanjani pale Tanga utakuta watu wanasomea ukocha wa mpira wa miguu. Mwalimu wao ni Oscar Mirambo, yule kocha wa Serengeti Boys iliyofeli nyumbani 2019. Hawa makocha wakihitimu ndiyo watapewa leseni zitakazokuwa juu ya leseni za UEFA zinazotolewa katika mafunzo yanayoendeshwa na vyama kama FA ya England pale Saint George Park, FFF ya Ufaransa pale Crairetountaine, DfB ya Ujerumani pale DFB Academy, La Ciudad del Fútbol ya RSFF ya Hispania au IFG ya Italia pale Coverciano.

Nimetolea mfano vituo hivyo ambavyo ni bora zaidi katika nchi hizo kubwa na zilizoendelea zaidi kisoka. Katika vituo hivyo, nchi hizo huendesha mafunzo ya hali ya juu ya ukocha na kutoa vyeti vya diploma mbalimbali.

Kwa elimu ya kawaida, vituo hivi tungeviita vyuo vikuu namba moja katika nchi zao. Na elimu inayotolewa hapo ndiyo elimu namba moja katika nchi zao. Halafu mtu aje kusema elimu inayotolewa kwenye vituo hivyo iko chini ya ile inayotolewa Afrika ikiwemo Tanzania.

Yaani UEFA A ya Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Italia au Hispania eti iko chini ya CAF A inayotolewa Tanzania. Huku ni kujidanganya kwa hali ya juu. Hivi kuna mzazi yeyote Afrika achilia mbali Tanzania anayeweza kukataa nafasi ya mwanaye kwenda kusoma Ulaya kwenye chuo namba moja eti kwa sababu elimu yao iko chini ya elimu ya Afrika?

Afrika, achilia mbali Tanzania haijawa bado na uwezo wa kuendesha mafunzo yoyote ya elimu iliyozaliwa Ulaya na kuwazidi wao. Bado sana. Kocha mwenye leseni A ya UEFA ana maarifa makubwa ya mpira kuliko mwenye CAF A kwa msingi wa mafunzo yao.

Kwa Afrika mafunzo yetu yako chini na yanaendeshwa kiujanjaujanja. Hatuna vifaa darasa, miundombinu, wakufunzi bora na wala hatujawekeza kwenye sayansi.

Kuwakataa makocha wa UEFA A kwa sababu ya CAF A ni kujidanganya pakubwa. Kwa hadhi ya madaraja CAF A iko sawa na UEFA A kwa sababu zote ni diploma za juu zaidi za mafunzo ya ukocha. Lakini kwa maarifa, UEFA A iko juu kutokana na mafunzo.

Hapa ndipo ninapomkumbuka Justin Kalikawe na wimbo wake wa UTARATIBU WETU.

Yaani tumejiwekea utaratibu utakaotufanya tubaki nyuma miaka mingi zaidi.

Kocha wa zamani wa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na Al Ahly ya Misri, Pitso Mosimane alitoa kauli ngumu yenye ukweli mchungu juu ya hili. Juni 2022, Pitso alikuwa Morocco kwenye masomo ya CAF Pro License ambayo ni ya kwanza Afrika, ikishirikisha makocha 23 tu.

Zaidi ya Pitso pia walikuwepo Aliou Cisse wa Senegal, Florent Ibenge wa DRC, Hoalid Regragui wa Morocco na kadhalika. Akiwa huko, Pitso alijifunza kitu kikubwa ambacho angependa kuona kinafanyika kwao Afrika Kusini.

Akizungumza na mtandao wa Independent Online (IOL) wa Afrika Kusini, Pitso alielezea namna alivyowaona watu wa Kaskazini mwa Afrika, hasa Morocco wakitumia maarifa ya Ulaya kukuza mpira wao akasema anatamani Afrika Kusini wangeiga hilo.

“I’ve been there for the last three years. You will be amazed to see what this country has done. They have the biggest vision ever and you come to my country, I’m sorry we are 20 years behind Morocco.” Akimaanisha.. “Nimekuwa kule kwa miaka mitatu. Utashangaa kuona nchi ile inavyofanya. Wana maono makubwa sana, lakini ukija nchini kwangu samahani kusema hili tuko miaka 20 nyuma yao.”

“The Moroccans are looking at this differently. They want their coaches in Europe, and in Europe, we can never have any excuses that we are not qualified.” Akimaanisha.. “Wamorocco wanaliangakia hili kwa jicho tofauti. Wanataka makocha wao wakasome Ulaya na Ulaya huwezi kuwa na visingizio kwamba eti hawana vigezo.”

Pitso, mmoja wa makocha wakubwa zaidi kuwahi kutokea Afrika anatamani nchi yake ifanye kama Morocco - kusomesha makocha wao Ulaya.

Halafu sisi Tanzania tunajidanganya kwamba makocha waliosoma Ulaya elimu yao haitoshi kulinganisha na waliosoma Afrika. Waliosoma Tanzania. Eti tunawasikiliza CAF. CAF hawana nchi wanayoiongoza wala hawana timu wanayoisimamia.

Mpira ukidorora Tanzania, CAF hawana mpango nao. Watashughulika na nchi nyingine kulikochangamka. Ni jukumu letu kuulinda mpira kwa kuhakikisha tunatumia makocha waliofundishwa vizuri ili kutufundishia wachezaji wetu. Hawa makocha wa CAF wanaopatikana Karume siyo wabaya acha wawepo, lakini tusiwadharau wenye UEFA A eti kwa sababu CAF A inatosha, hapana. Haitoshi.

Hebu ona hili, kocha wa zamani wa Simba, Didier Da Rosa, raia wa Ufaransa alipatwa na shida kama hiyo ya kukosa vigezo kwa kuwa alikuwa na UEFA A, badala ya kuwa na CAF A. Akashindwa kuiongoza Simba kwenye Ligi ya Mabingwa. Akaondoka.

Lakini akaenda kuwa kocha wa timu ya taifa ya Mauritania na akaiongoza kwenye Afcon. Sasa utaona CAF walivyo wanafiki. Afcon ndiyo mashindano makubwa zaidi na ndiyo yangehitaji makocha wenye vigezo zaidi, lakini hawana habari.

Kwa hiyo Tanzania kuiga kama lilivyo kutoka CAF ni kujidanganya sana. Ndiyo maana timu kama Azam FC imemuajiri Yousouph Dabo mwenye Diploma A ya UEFA kama kocha mkuu, lakini wakapeleka jina lake TFF na CAF kama kocha msaidizi.

Lengo ni kuikwepa hii sheria ya hivyo. Watu wanaajiri maarifa siyo cheti.

Endelea kupumzika kwa amani Justin Kalikawe.

Chanzo: Mwanaspoti