Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shangwe la Ubingwa Yanga angani

Mashabiki Yanga Shangwe Shangwe la Ubingwa Yanga angani

Sat, 13 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Huko Italia kuna balaa la mashabiki. Napoli wanashangilia ubingwa wao wa tatu wa ligi walioumisi kwa miaka 33 ambapo wanashangilia kwa aina tofauti kidogo, ikiwemo kukodi ndege na kushangilia angani. Sasa Yanga nayo imepanga kulifanya leo kama itautwaa kwa mara ya 29.

Iko hivi. Baada ya matokeo ya jana ya Simba na Ruvu Shooting, Yanga inahitaji ushindi katika mechi ya leo dhidi ya Dodoma Jiji ili itangazwe mabingwa wa msimu huu, kwani itafikisha alama 74 ambazo hakuna timu yoyote inayoweza kuzifika katika Ligi Kuu Bara.

Huko kambini unaambiwa morali ya wachezaji, viongozi na benchi la ufundi ipo juu na wamepania kushinda leo ili watawazwe mabingwa na baada ya hapo wakashangilie hewani, kwani baada ya mechi kumalizika kikosi kitasafiri kwa ndege kwenda Afrika Kusini kuvaana na Marumo Gallants katika mechi ya marudio nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya ushindi wa 2-0 nyumbani.

Licha ya Dodoma iliyo nafasi ya 10 katika msimamo ikiwa na pointi 31 imepanga kutibua shangwe hilo la Wananchi kwa kushinda leo, lakini bado rekodi haziibebi kwani imekutana mara tano na Yanga na imefungwa mara nne na kutoa sare mara moja tu.

Kama Yanga itashinda mechi ya leo basi, wakati baadhi ya mashabiki zake wakiendelea kushangilia nchini, wengine watakuwa angani sambamba na kikosi kizima wakishangilia kutoka Dar es Salaam hadi Johannesburg, weanapoifuata Marumo kwa mechi itakayopigwa Jumatano ijayo huko Sauzi.

Vaibu hilo litakolezwa na mabosi wa juu wa Yanga, ambapo Makamu wa Rais, Arafat Haji aliliambia Mwanaspoti wanataka kubeba ubingwa leo ili waende Sauzi kwa shangwe na morali ya juu.

"Tunataka kabla ya kwenda Afrika Kusini tuchukue kwanza taji la pili msimu huu kwa kubeba Kombe la Ligi ili twende huko tukiwa na shangwe la kutosha," alisema Arafat na kuongeza;

"Tukishinda hapa tutakuwa na morali ya juu, pia itatusaidia kwenye mechi yetu na Marumo kwani na kule tunataka kupata matokeo yatakayotuvusha hadi fainali, hivyo mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi uwanjani kuisapoti na kuwa sehemu ya historia hii ya aina yake."

Akizungumzia mechi dhidi ya Dodoma, Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi alisema ni muhimu sana kwa timu, kwani lengo ni kushinda na kubeba ubingwa kabla ya kwenda Afrika Kusini na kutakuwa na mabadiliko katika kikosi.

"Tunataka kushinda ili tubebe ubingwa wa pili mfululizo wa ligi. Tunawaheshimu Dodoma, lakini tunachohitaji ni kushinda ili tuende kwenye mechi na Marumo tukiwa na morali nzuri.

"Kutakuwa na mabadiliko kikosini, ila hiyo sio sababu ya kushindwa kushinda kwani kila mchezaji yupo hapa ili kuhakikisha Yanga inashinda na kufikia malengo," alisema Nabi. Kwa upande wa kocha msaidizi wa Dodoma, Kassim Liyogope alisema watacheza mechi hiyo kwa nidhamu na lengo ni kupata ushindi ili kusogea juu kwenye msimamo.

"Tunatambua ubora wa Yanga, itakuwa ni mechi ngumu lakini tumejipanga kwa lengo la kuhakikisha tunshinda na kupanda katika nafasi za juu kwenye msimamo," alisema Liyogope.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: