Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shamte kuikosa Kagera Sugar, Ntibazonkiza wenzake freshi

Shamteeeeeee Shamte kuikosa Kagera Sugar, Ntibazonkiza wenzake freshi

Mon, 5 Sep 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Beki wa kulia wa Geita Gold, Haruna Shamte anatarajiwa kuwa mchezaji pekee wa timu hiyo atakayekosekana kwenye mchezo wa kesho dhidi ya Kagera Sugar huku nyota mpya, Saido Ntibazonkiza na wenzake wa kimataifa waliokosekana katika michezo miwili ya kwanza wakiwa fiti kukiwasha kesho.

Mchezo huo wa Ligi Kuu utachezwa saa 10 jioni katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa baada ya uwanja wa nyumbani wa Geita Gold, Nyankumbu uliopo mkoani Geita ukifanyiwa maboresho.

Akizungumzia maandalizi ya kikosi chake katika mkutano na waandishi wa habari jijini hapa leo Septemba 5, Kocha Msaidizi wa Geita Gold, Mathias Wandiba amesema Shamte aliumia katika mchezo dhidi ya Simba na atakosekana kesho lakini nyota wengine wote akiwemo Ntibazonkiza, Arakaza McAthur, Shown Oduro na wachezaji wengine wa kimataifa waliokosekana katika mechi mbili za kwanza watakuwepo.

Amesema timu yao imepata muda mzuri wa kujiandaa dhidi ya Kagera Sugar ambapo lengo kuu la wachezaji na benchi la ufundi ni kupata alama tatu ili kuanza vyema raundi ya tatu baada ya kupoteza michezo miwili ya awali.

"Tunakwenda kukutana na timu iliyobora mchezo utakuwa mgumu lakini benchi la ufundi na wachezaji tumejiandaa kuhakikisha tunapata alama tatu katika uwanja wetu wa nyumbani, tumewaandaa wachezaji kisaikolojia na kiufundi ili kufanya vyema na wako tayari,"

"Kesho tutamkosa Haruna Shamte wachezaji wengine wote wa kigeni watakuwepo kila mchezaji tuliyemsajili yuko tayari ni sisi kuamua tu tunamtumia nani na hatuna wasiwasi na mchezaji yoyote," amesema Wandiba.

Nahodha wa kikosi hicho, Geofrey Manyasi amesema wachezaji wako tayari kupambana kesho kuipa pointi tatu timu yao kwani benchi la ufundi limewaandaa kiakili na kimwili ambapo wamekubaliana kwa ajili ya malengo ya timu kuipatia ushindi kesho.

Katibu wa Chama cha soka Mkoa wa Mwanza (MZFA), Leonard Malongo ametaja viingilio vya mchezo huo ni Sh 10,000 (VIP A), 5,000 (VIP B) na 3,000 kwa mzunguko ambapo amewataka mashabiki kununua tiketi mapema kujitokeza kwa wingi katika mchezo huo ambao ni wa kwanza wa ligi msimu huu katika Uwanja wa CCM Kirumba.

Chanzo: Mwanaspoti