Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi akwamisha kesi ya Malinzi

Tue, 18 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Jumanne, Desemba 18, 2018 , imeshindwa kuendelea kusikiliza ushahidi katika kesi ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa dola 173,335 za Marekani na Sh43,100,000, inayomkabili, Jamal Malinzi na wenzake wanne.

Kesi hiyo imeshindwa kuendelea leo Jumanne Desemba 18, 2018 baada ya shahidi wa 10 kutofika mahakamani kwa kile kilichodaiwa ana matatizo ya kifamilia.

Tayari mashahidi tisa wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa hao, akiwemo  Malinzi aliyekuwa rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Mwendesha mashtaka wa Takukuru, Leonard Swai ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi lakini shahidi  waliyemuandaa amepata matatizo ya kifamilia.

Wakili wa utetezi Abrahamu Senguji amedai kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuandaa mashahidi hivyo walitakiwa kuandaa shahidi zaidi ya mmoja.

"Rekodi za mahakama ziliutaka upande wa mashtaka kuleta mashahidi watatu, sisi upande wa utetezi tunasema upande wa mashtaka wameshindwa kuandaa shahidi tunaona hawana nia ya kuendelea na kesi hii hivyo mahakama inaweza kuiondoa kesi hii na kuwaachia huru," amedai wakili Senguji.

Baada ya kuelezwa hayo,  Hakimu Mashauri alikubaliana na upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Januari 2, 2018 na kusikilizwa kwa mfululizo Januari 16, 17 na 21, 2019 huku akiutaka upande wa mashtaka kuandaa mashahidi.

 

Mbali na Malinzi, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa  Selestine (46) na mhasibu wa TFF,  Nsiande  Mwanga(27).

 

Wengine ni Meneja wa  ofisi TFF, Miriam Zayumba na Karani wa shirikisho hilo, Flora Rauya ambao kwa pamoja  wanakabiliwa na mashtaka 30 katika  kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha wa dola za Marekani 173,335 na Sh 43,100,000.



Chanzo: mwananchi.co.tz