Mchambuzi nguli wa masuala ya soka nchini, Shaffih Dauda amewaponda baadhi ya mashabiki wa Klabu ya Simba ambao wamekuwa na tabia ya kulalamika kuwa timu yao inacheza vibaya licha ya kupata matokeo mazuri.
Dauda amesema hayo wakati akizungumza kupitia Hili Game ya Clouds FM kufuatia matokeo ya jana ya Simba ya bao 3-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga katika Dimba la Uhuru, Dar es salaam.
“Kinachowavuruga mashabiki wa Simba ni ujivuni wa mashabiki wa Yanga, kwa sasa mashabiki wa Yanga wanaongoza kwa makelele mitandaoni wakijivunia ubora wa timu na wachezaji wao.
"Hii imegeuka kutoka kipindi kile ambacho mashabiki wa Simba walikuwa wakiwatambia wenzao wa Yanga! Simba walikuwa wanasema wenyewe wanapiga 'Pira Biriani' halafu Yanga wanapiga 'Pira Gimbi'.
"Wanaoangalia mechi za Simba kiufundi wanaelewa na hawaoni shida kwa namna Simba inavyokwenda, ila mashabiki wa Simba wao wanataka kuona timu yao inapiga pasi nyingi na kufunga magoli mengi kama Yanga ilivyoanza.
"Sioni sababu za mashabiki wa Simba kulaumu wachezaji na kocha wao, wameshinda mechi zote tatu za Ligi, wana alama tisa sawa na Yanga na Azam, wamefunga magoli tisa wameruhusu magoli mawili
"Ukimuuliza huyo shabiki anaelalamika anataka nini? Atakwambia Simba haichezi vizuri, muulize tena kucheza vizuri ni kupi? Halafu subiri majibu yake,” amesema Shaffih Dauda.