Feisal Salum ‘Feitoto’ namba zake zinaongea vizuri sana, amefunga magoli 12 na kutoa pasi tano zilizozaa magoli ‘assists’. Yeye ndio kinara kwenye orodha ya wafungaji wa Ligi hadi sasa.
Inavyoonekana Feitoto hawekwi kwenye orodha ya wachezaji wanaofanya vizuri kwenye Ligi, hana wazungumzaji wengi kwa maana ya mashabiki.
Mara nyingi Azam ikizungumzwa basi inazungumzwa na waandishi wa habari lakini sio mashabiki wa mchezo wenyewe.
Kwa hiyo unakuta habari za Feitoto kufanya vizuri sio kubwa mitaani lakini msimu huu umemuwa bora kwake. Namba alizonazo hadi sasa pengine hajawahi kuwa nazo tangu ameanza kucheza Ligi Kuu ya bara [kuhusika kwenye magoli 17] huku msimu ukiwa bado haujamalizika.
Anastahili pongezi kwa hiki anachokifanya, ukitazama mapito aliyopitia kabla ya kujiunga na Azam usingetarajia kama angeweza kuwa katika ubora huu kwa haraka kiasi hiki.
Msimu bado haujamalizika, Feitoto anaweza kufanya vizuri zaidi ya hapa. Mwalimu wa Azam anamtumia Feitoto nyuma ya mshambuliaji kiongozi, kwa hiyo mara nyingi anafika kwenye eneo la box la wapinzani.