Mwanamke mwenye umri wa miaka 31 wa eneo la Ndola Northrise amefariki dunia ghafla kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa juzi alipokuwa akiwatazama mabingwa wa Zambia, Power Dynamos wakimenyana na wababe wa Tanzania Simba FC katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa Raundi ya Pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Angela Mwape akiwa stendi na mumewe Stanely Mwamba Mpundu na mtoto wao mchanga walikuwa wakitoka eneo walilokuwa na kujaribu kusogea eneo jingine ambako kulikuwa na wanawake wenzake wanaofahamiana.
Kwa mujibu wa mashuhuda, Angela alianguka wakati akielekea kwa wanawake hao na kukimbizwa katika Hospitali ya Mafunzo ya Ndola ambako alifikwa na mauti alipowasili.
Kifo cha Angela kiliacha mume wake ambaye wameishi naye kwa miaka miwili, huku familia na marafiki wakigubikwa na huzuni na majonzi makubwa.
Mwanafamilia mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe kwenye vyombo vya habari, amethibitisha kifo cha Angela.
Katika mchezo huo, Simba ilifanikiwa kutoa sare ya bao 2-2 na Power Dynamos na wanatarajia kurudiana Oktoba 1, 2023 jijini Dar es Salaam.