Mchezo wa Ligi Kuu Uhispania kati ya wenyeji Granada dhidi ya Athletic Bilbao umelazimika kuahirishwa baada ya kifo cha shabiki wa Granada katika dimba la Nuevo los Cármenes.
Athletic walitangulia kupata bao la mapema kupitia kwa Inaki Williams, kabla ya mchezo kusimamishwa baada ya takriban dakika 15 pale Mwamuzi alipoarifiwa kuhusu tatizo jukwaani.
Wakati shabiki huyo akiendelea kupatiwa matibabu wachezaji walitolewa nje ya uwanja lakini baadaye LaLiga ilithibitisha kuwa shabiki huyo amefariki na mechi itapangwa tena siku za usoni.
Taarifa ya klabu ya Athletic Bilbao imesema “LaLiga na vilabu vyote viwili vimekubali kusitisha mechi kutokana na kifo cha shabiki dimbani Los Carmenes.
“Klabu ya Athletic inatoa rambirambi zake za dhati. Mawazo yetu yapo kwa familia ya mtu huyo na wapendwa wake.”