Msanii maarufu wa komedi, Mboto Haji ambaye pia ni shabiki kindakindaki wa Klabu ya Yanga amesema kuwa kwa kiwango inachoonesha timu yake kwa sasa, wanaomba mechi ya marudiano dhidi ya Al-Merrikh ipelekwe nchi yoyote, Wananchi watashinda.
Mboto amesema hayo mara baada ya kikosi cha Yanga kuibuka na ushindi wa bao 2-0 wakiwa ugenini Kigali nchini Rwanda juzi, Jumamosi, Septemba 16, 2023 dhidi ya Al-Merrikh kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
"Mechi ya marudiano sisi tutawasikiliza CAF wanatuambiaje, kama Kagame atasema tucheze hapa Rwanda, au Rais wa Burundi akasema mechi ikachezwe kwake tutakwenda,
"Sisi tunachohiaji ni kuzunguka Afrika Mashariki. Tukiambiwa mechi ikachezwe Eritrea au Ethiopia tutakwenda, tutacheza na tutapata ushindi.
"Sisi tunaangalia wapi viongozi watatupeleka. Natamani viongozi wetu waseme kwamba uwanja wetu umeleta shida na nyasi ziliondoka ghafla, kwa hiyo watupangie hata Eritrea twende tukachezee kule," amesema Mboto Haji.
Si mara ya kwanza kwa Yanga kushinda ugenini kwenye michuano ya CAF, ilifanya hivyo msimu uliopita dhidi ya Zalan (0-4), Club Africain (0-1), Real Bamako (0-2), Marumo Gallants (0-2), TP Mazembe (0-1), USM Alger (0-1). Msimu huu Yanga imeshinda dhidi ya ASAS FC (0-2), Al-Merrikh (0-2).
Mechi ambazo Yanga imepoteza ugenini ni mbili tu tangu msimu uliopita kwenye mashindano ya CAF, dhidi ya Al-Hilal ya Sudan (1-0) na dhidi ya Monastir ya Tunisia (2-0).