Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shabiki Arsenal auwawa, kipigo Man United chatajwa

Arsenal Kit 2020 211595512935684 Shabiki Arsenal auwawa, kipigo Man United chatajwa

Tue, 5 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Polisi wilayani ya Sheema, magharibi mwa Uganda, wanamsaka kijana mwenye umri wa miaka 22, anayetuhumiwa kwa mauaji ya shabiki wa Arsenal ambaye ni mkazi wa Rwanyinakahire, Kata ya Rwamujojo, wilayani humo Jackson Aineruhanga.

Tarifa ya Polisi imeeleza kuwa kijana huyo ambaye jina lake halijawekwa wazi, anadaiwa kumuua Aineruhanga kwa kuchoma na kisu muda mfupi baada ya ushindi wa Arsenal wa 3-1 dhidi ya Manchester United.

"Inadaiwa kuwa jioni ya Septemba 3, 2023, kulitokea kutokuelewana kati ya wawili hao, walipokuwa wakitazama mechi hiyo ya Ligi Kuu England" amesema Msemaji Mkuu wa Polisi wa Bushenyi, Marcial Tumusiime

Kwa mujibu wa msemaji huyo, mabishano ya mashabiki hao wa soka yalianza baada ya bao la dakika za lala salama la Alejandro Garnacho wa Manchester United kufutwa kwa sababu ya kuotea iliyoamuliwa na teknolojia ya VAR.

"Baadaye wawili hao walienda kwenye baa moja lakini walifukuzwa kwa sababu kuendelea kuzozana, jambo hilo lilisababisha mtuhumiwa kumchoma Aineruhanga, na kitu chenye ncha kali kifuani, ambapo baada ya shambulio hilo, alitokwa na damu nyingi na hivyo kusababisha umauti," amesema Tumusiime.

Baada ya tukio hilo, mtuhumiwa anadaiwa kukimbia, hata hivyo, Polisi imetembelea eneo la tukio ambapo wamekusanya ushahidi ikiwa ni pamoja na kipande cha fimbo kilichokuwa na madoa ya damu pamoja na viatu vya mtuhumiwa.

“Mwili wa Aineruhanga baadaye ulipelekwa katika Kituo cha Afya cha Kabwohe IV kwa ajili ya uchunguzi," amesema Kamanda Tumusiime.

Chanzo: Mwanaspoti