Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sh2 bilioni za Mayele zinaweza kufanya haya

Mayele Bora Fiston Mayele

Tue, 22 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Fiston Mayele ameshaanza kupiga mzigo katika timu yake mpya ya Pyramids ya Misri, baada ya kuitumikia klabu ya Yanga kwa misimu miwili yenye mafanikio makubwa, akibeba mataji sita na tuzo za Mchezaji na Mfungaji Bora.

Mayele amesajiliwa na Pyamids kwa kitita kinachosemakana cha Sh2 bilioni na baada ya kutambulishwa alirudi Tanzania kuichukua familia yake na alienda kupata dua kwa Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar, Walid Alhad Omar.

Mayele ameondoka nchini akiwa amefunga jumla ya mabao 33 ya Ligi Kuu Bara na mengine 14 ya kimataifa ya CAF na sasa ameanza maisha mapya Misri anakoenda kucheza kwa mara ya kwanza.

Mayele atakumbukwa na Wananchi kwa kile ambacho alikifanya ndani ya msimu miwili aliyoichezea Yanga, alianza na mabao 16 kwenye Ligi Kuu Bara msimu wa kwanza na kukikosa kiatu cha dhahabu kilichokwenda kwa George Mpole aliyekuwa Geita Gold akifunga mabao 17 na katika msimu wa pili Mayele alitupia mabao 17 na kumaliza kinara akilingana na Saido Ntibazonkiza wa Simba.

Msimu uliopita, alifunga mabao mengine 14 katika mashindano ya CAF, akianza na saba ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua za awali kisha mengine kama hayo kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ambapo Yanga ilifika fainali dhidi ya USM Alger ya Algeria. Mayele ameondoka Yanga baada ya kuisaidia kutwaa taji la Ligi Kuu mara 2, Kombe la ASFC (2) Ngao ya Jamii mara mbili na kuisaidia Yanga kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza katika historia yao msimu 2022/2023 na ndio Mfungaji bora wa Michuano hiyo akimaliza na mabao 7.

Wakati kocha wa Yanga, Miguel Gamondi akiwa na jukumu la kusuka upya safu yake ya ushambuliaji haya ndio mambo unayoweza kufanya kutokana na mkwanja ambao Pyramid FC umeutoa kwa Yanga ili kupata huduma ya Mayele ambaye pia atakumbukwa kwa staili yake kushangilia ya kutetema.

Kama ulikuwa hujui ni kwamba fedha za usajili wa Mayele kwenda Pyramids zinaweza kufanya mambo kibao, kwani ni mkwanja mrefu kwelikweli Kibongobongo na hapa chini ni baadhi ya mambo yanayowezwa kufanywa na minoti hiyo;

KILA MCHEZAJI ANAPATA GARI

Mkwanja ambao Waarabu wametoa kwa Mayele unatosha na chenji inabakia kama uongozi wa timu hiyo ungeamua kuwanunulia kila mchezaji kwenye kikosi chao gari aina ya Kia K5 LX ambayo inatoka mwakani 2024.

Gharama za KIA K5 LX moja ni zaidi ya 55.3 milioni kwa wachezaji 30 wa kikosi cha kwanza, kiasi ambacho kinaweza kutumika hapo ni zaidi ya Sh1.6 bilioni na mkwanja ambao utasalia unaweza kutumika kwa upande wa benchi la ufundi ambalo linaongozwa na Miguel Gamondi.

Kama uongozi utaamua ununue IST basi hiyo itakuwa neema kwa vikosi vyote vya Yanga kuanzia kikosi cha kwanza cha wachezaji 30, Yanga B nao 30 na upande wa Yanga Princes 30 pamoja na mabechi yao yote ya ufundi na bado chenji itabaki kwa hesabu ya IST moja iwe na thamani ya Sh15 milioni.

Kwa wachezaji 90 au tufanye hata 100 inapata zaidi ya Sh 1.5 bilioni kwenye mkwanja wa Mayele ingesalia Sh500 milioni ambazo unaweza kununua magari kwa mabechi yao yote ya ufundi na bado mzigo wa usajili wa Mayele ungebaki.

BODABODA 800

Kitita cha usajili wa Mayele kinaweza kutumika kununua zaidi ya bodaboda 800 kwa hesabu ya boda moja kuwa na thamani ya Sh 2.5 milioni.

Rejesho ya boda moja kwa siku ni Sh10,000 hesabu ya wiki ni Sh70,000 kwa mwaka ni Sh3,640,000 hivyo usajili wa Mayele unaweza kuzalisha faida ya zaidi ya Sh900milioni kwa kukokotoa kwa boda 800 ambazo unaweza kununua kwa pesa yake ya usajili ambayo Yanga imevuna.

NYUMBA KWA WACHEZAJI

Mkwanja wa usajili wa Mayele unatosha kwa kila mchezaji wa kikosi cha Yanga kupata nyumba yenye thamani ya Sh66.6 milioni ambayo inakuwa inakuwa na vyumba vinne vya ikiwemo (master bedroom) moja na sitting room, dinning, jiko na choo na bafu za pamoja.

Kwa mujibu wa Injinia Innocent Kapama mkwanja huo unatosha kujenga nyumba yenye thamani hiyo kulingana na uzoefu wake.

“Unaweza kujenga nyumba nzuri tu na kuondokana na maisha ya kupanga,” anasema Injinia huyo.

Kwa idadi ya wachezaji 30 yaani kila mmoja apate nyumba yenye thamani ya 66.6 milioni unapata mkwanja ambao Waarabu wametoa kwa Mayele.

BAJETI YA COASTAL

Fungu la usajili wa Mayele ni bajeti ya msimu ujao kwa baadhi ya klabu za Ligi Kuu Bara ikiwamo Coastal Union ya Tanga na chenji inabaki.

Wiki chache zilizopita Katibu Mkuu wa Coastal, Omary Ayoub aliweka wazi kuwa bajeti yao kwa msimu huu ni Sh1.5 bilioni hivyo fungu la usajili wa Mayele linaweza kutumika kuiendesha timu hiyo na zaidi ya Sh500 milioni zikasalia.

MGAWO KWA MKAPA

Kuonyesha wingi wa mkwanja wa usajili wa Mayele ukisema uugawe unaweza kumpa Sh33,000 kila shabiki ambaye ataingia kwenye uwanja wa Benjamani Mkapa wenye uwezo wa kuingiza watu 60,000.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: