Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sh11 milioni zatajwa kuiua Mbeya City

Mbeya City Mill 11 Sh11 milioni zatajwa kuiua Mbeya City

Fri, 30 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati wadau na mashabiki wa Mbeya City wakijiuliza mzimu unaowatesa kwa sasa wa kutokuwa na matokeo mazuri, mapya yameibuka ikielezwa sababu inayochangia wachezaji kushuka morali.

Mbeya City ambayo ilikuwa na mwanzo mzuri kwenye Ligi Kuu, kwa sasa hali imekuwa si shwari kutokana na kucheza mechi tisa mfululizo bila kuonja ushindi, huku kwenye uwanja wa Sokoine hali ikiwa tete zaidi.

Katika michezo iliyocheza nyumbani kwenye uwanja huo, Mbeya City imeshinda miwili tu kati ya 12 iliyocheza, sare nane na kupoteza miwili na kuwa nafasi ya 10 kwa pointi 12.

Mmoja wa watu wa ndani (jina tunalo) alisema kinachoidhoofisha timu hiyo ni uongozi kutotimiza ahadi kwa wachezaji kwenye ishu ya bonasi ambayo ni zaidi ya mechi sita sasa.

Alisema kwa sasa takribani Sh 11 milioni zinadaiwa na wachezaji kwani mara ya mwisho bonasi zao zilitolewa mechi yao dhidi ya Mtibwa Sugar Oktoba 2, walipotoa sare ya mabao 2-2.

“Posho ndizo zinaendesha maisha ya wachezaji kununua hata vocha na familia, kutegemea mshahara peke yake haiwezi kusaidia kitu, ukiangalia moto tulioanza nao kwa sasa morali imeshuka,” alisema na kuongeza:

“Suala la mshahara hakuna madai kwa sababu hata Desemba, mzigo uliingizwa tarehe 24, japokuwa kuna kipindi nyuma ilichelewa takribani miezi mitatu, hivyo nadhani hii ndio shida.”

Kwa upande wake kocha msaidizi wa timu hiyo, Anthony Mwamlima alisema benchi la ufundi limekuwa na muda mwingi kufanya kazi yao, lakini wachezaji wameshindwa kulinda viwango vyao.

“Sijui wamelewa sifa, kwa sasa ukiangalia mchezaji mmoja mmoja viwango vimebadilika sana, ile kasi yao imepotea wameshindwa kulinda ubora wao,” alisema Mwamlima.

Mwenyekiti wa timu hiyo, Joseph Mlundi alikanusha taarifa hizo akibainisha kuwa msimu huu klabu imekuwa makini sana kujali maslahi ya wachezaji na kwamba hakuna madai yoyote akisema hata mechi yao na Simba walitoa bonasi Sh10 milioni.

“Hata sisi tunajiuliza kinachowashusha morali vijana, hata kama ingekuwa tunadaiwa bonasi kwani zipo kwenye mkataba? Hizo ni mapenzi ya mwajiri kutoa au kutotoa, ila uongozi unaendelea na mikakati kurejesha ari upya,” alisema Mlundi.

Chanzo: Mwanaspoti