Viwanja saba vya soka vitaanza kufanyiwa marekebisho baada ya tathmini kukamilika.
Viwanja hivyo ni vile ambavyo vilitengewa Sh10 bilioni katika bajeti ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ya mwaka 2022/2023.
Viwanja vitano kati ya saba vinamilikiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) na vingine ni kile cha Uhuru na Mkapa.
Akizungumza Katibu Mkuu wizara hiyo, Said Othman Yakub alisema baada ya kuidhinishiwa fedha hizo, walimpata mkandarasi mshauri ambaye ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), aliyezunguka katika viwanja vyote vinavyotarajiwa kufanyiwa maboresho kuangalia kinachopaswa kufanyika.
“Kwa hatua ya kwanza ya ukarabati vitaanza viwanja saba vilivyopo katika majiji, ambavyo ni Jamhuri (Dodoma), Sheikh Amri Abeid (Arusha), Sokoine (Mbeya), CCM Kirumba (Mwanza) na Mkwakwani (Tanga), lakini ukarabati huo utavihusisha viwanja vya Uhuru na Benjamin Mkapa.
“Kuna maboresho makubwa yatafanyika katika viwanja hivi, baadhi vitaongezewa majukwaa, vingine vitaboreshewa vyumba vya kubadili nguo wachezaji na vingine vitaboreshewa nyasi za uwanja (pitch),” alisema Yakub.
Alisema uwanja kama wa Benjamini Mkapa utajengwa na wakandarasi wawili huku mmoja akiwa wa kimataifa ili kuupa hadhi kubwa.
“Uwanja wetu kwa sasa unaweza kutumika katika michuano ambayo Simba na Yanga zinashiriki, lakini Super League ambayo Simba imechaguliwa kushiriki hauwezi kutumika kwa sababu ina viwango vikubwa hivyo tunataka kuufanyia maboresho zaidi.”