Ligi Kuu ya Zanzibar iliyokuwa imepangwa kumalizika jana imesimamishwa ili kutoa nafasi kwa rufaa iliyokatwa na Black Sailor FC inayopingwa kupokonywa pointi katika mechi yao dhidi ya KMKM ambayo haikumalizika, imefahamika.
Mechi ya Ligi Kuu Zanzibar kati ya Black Sailor dhidi ya KMKM ilivunjika kutokana na kitendo cha wachezaji wa Black Sailor kumpiga mwamuzi baada ya wapinzani wao kusawazisha bao dakika ya 83 na kufanya matokeo kuwa sare ya bao 1-1.
Bingwa wa ligi hiyo inayotoa mwakilishi wa Zanzibar katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika na inadhaminiwa na PBZ ilitarajia kupata bingwa wake katika mechi hizo za funga pazia.
Akizungumza na Nipashe, Katibu wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Hussein Ahmada Vuai, amesema wamepokea barua kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Michezo Zanzibar ikieleza imesimamishwa michezo mitano ya kufunga rasmi pazia la Ligi Kuu ya Visiwani hapo mpaka rufaa ya Black Sailor itakapofanyiwa kazi.
Vuai amesema Black Sailor inapinga uamuzi uliotolewa na Bodi ya Ligi pamoja na Kamati ya Rufaa na Usuluhishi ya ZFF ambayo iliipokonya pointi timu hiyo na kuwapata alama tatu KMKM.
"Kamati zote mbili hazikutakiwa kusikiliza shauri hilo na badala yake Kamati ya Nidhamu ndio ilikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na kutoa uamuzi kwa mujibu wa Katiba ya ZFF," imesema sehemu ya barua ya msajili huyo.
Maafande wa KMKM na KVZ, ndio wanachuana katika mbio za kuwania taji hilo.