Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yaja juu vurugu viwanjani

2a6009df201203495e5b533ab0f68188 Serikali yaja juu vurugu viwanjani

Wed, 30 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI imeliagiza Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuchukua hatua kali kwa watakaoendeleza vurugu uwanjani.

Kauli hiyo inakuja ikiwa ni siku chache zimepita tangu kutokee vurugu za mashabiki wa Yanga waliowafanyia wale wa Simba katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar, kitendo kinachoonekana kujirudia baada ya kuwahi kutokea kabla Dar es Salaam.

Akizungumza na Azam Media, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Dk Yusuf Singo alisema anajua kuwa tayari taasisi na klabu zilitoa maonyo ila wao kama serikali wameona pia wakemee ili vitendo hivyo vya kuvunja amani visijirudie.

“Tunajua taasisi zinazohusika pamoja na klabu zimekuwa zikitoa maonyo, tunajua pia TFF na BMT walikemea na serikali tunakemea mashabiki wote wanaovunja amani,”alisema.

Alisema kama vitendo hivyo vitajirudia TFF na BMT watumie kanuni na sheria zilizopo kuwachukulia hatua kali kwa wale watakaohusika ili kuvunja utamaduni huo unaotaka kujengeka.

Katika hatua nyingine, beki wa kati wa Yanga Lamine Moro aliwahimiza mashabiki wa soka nchini kuwa kitu kimoja na kusisitiza kuwa mpira sio uadui.

Moro alizungumza hayo juzi baada ya kuongezewa mkataba wa miaka miwili utakaomalizika mwaka 2023 ikidaiwa aliokuwa nao ulikuwa unakwenda ukingoni.

Alisema, “mpira sio vita, ni upendo. Napenda kuwahimiza mashabiki wote wa soka tuwe kitu kimoja hivyo, hauwezi kutufanya kuwa maadui, tujaribu kushirikiana kwani baada ya mpira kuna familia,”alisema.

Mchezaji huyo raia wa Ghana alisema watu wanapaswa kujaribu kudhibiti baadhi ya vitu vibaya hasa wanapokuwa uwanjani.

Beki huyo anakuwa mchezaji wa kwanza kujitokeza hadharani kukemea vurugu za mashabiki na kusisitiza umoja.

Mbali na hilo, aliushukuru uongozi wa Yanga na mashabiki kwa kumuamini na kumuongezea mkataba akiahidi kuwafurahisha zaidi katika michezo ijayo.

Chanzo: habarileo.co.tz