Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imetoa ufafanuzi kuhusu picha na taarifa inayosambaa katika Vyombo vya Habari na Mitandao ya Kijamii yenye kichwa cha habari 'Uwanja wa Mkapa Unaanza Kutia Aibu’ ambapo imesema picha zinazotumika pamoja na ujumbe ho ni picha ambazo zilichukuliwa siku za nyuma (mara baada ya tukio la Mkesha lililofanyika tarehe 16/12/20 katika uwanja huo).
“Kufuatia hali hiyo iliyojitokeza wakati huo, Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ilichukua hatua mbalimbali ili kuhakikiksha kuwa hali hiyo haijitokezi tena ambapo Wizara ilifanya mabadiliko ya Menejimenti ya Uendeshaji wa Uwanja huo.
“Wizara pia kwa kushirikiana na Bodi ya Ligi ambayo ndiyo Mdau mkubwa imeandaa muongozo wa matumizi wenye lengo la kudhibiti masuala ya usafi, Wizara imeunda pia kikosi kazi kidogo cha usafi na mazingira ambacho kinafanya ukaguzi wake kabla na baada ya uwanja kutumika ili kuimarisha usafi na Wizara limuelekeza Mzabuni wa uwanja huo kuboresha huduma ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya vibarua wa usafi wakati wa matukio”
“Wizara inatoa rai kwa Wadau wa michezo na umma wote wa Watanzania kushirikiana katika kuvitunza viwanja vyote kwa kuzingatia usafi wakati wa matumizi yake na kujiepusha na aina yoyote ya uharibifu”