Beki kutoka nchini Hispania Sergio Ramos anatarajia kujiunga kwenye mazoezi ya kikosi cha kwanza cha klabu yake ya Paris Saint-Germain, kuanzia juma lijalo, baada ya kupona majeraha ya ‘Kiazi cha Mguu’, huku kiungo kutoka nchini Italia Marco Verratti, akitarajiwa kuendelea kuwa nje ya dimba kwa karibia mwezi mmoja.
Beki huyo aliyeondoka Real Madrid mwishoni mwa msimu uliopita, alisajiliwa huko Parc des Princes, sambamba na Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Argentina Lionel Messi, Mlinda lango kutoka nchini Italia Gianluigi Donnarumma, Kiungo kutoka Uholanzi Georginio Wijnaldum na Achraf Hakimi kutoka Morocco.
Mpaka sasa Ramos bado hajacheza mchezo wowote tangu alipojiunga na PSG, kufuatia kuumia ‘Kiazi cha Mguu’ mwishoni mwa Julai.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo ya jijini Paris- Ufaransa zimethibitisha kwamba, Ramos atajiunga na wachezaji wenzake katika mazoezi ya pamoja baada ya kupona, ili aweze kuanza kucheza.
“Sergio Ramos alikuwa kwenye programu maalumu na timu ya madaktari na sasa ameruhusiwa kuanza mazoezi,” ilisema taarifa ya klabu hiyo kupitia kwenye tovuti yake.”
“Anatarajia kuanza mazoezi pamoja na kikosi cha kwanza juma lijalo.”
“Lakini Verratti atakuwa nje karibu mwezi mmoja baada ya kuumia nyonga na ana uwezekano wa kukosa michezo mitano ya PSG kwenye mashindano yote zikiwamo mbili za Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya RB Leipzig na Manchester City.” Imeeleza taarifa hiyo.
PSG kwa sasa inaongoza msimamo wa Ligi Daraja la Kwanza nchini Ufaransa ‘Ligue 1’ kwa kufikisha alama 28, huku kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya ikiongoza msimamo wa Kundi A, kwa kufikisha alama 7.
Kundi A la michuano hiyo lina timu kama RB Leipzig, Club Brugge na Manchester City.