Mashabiki wa soka kwa sasa wamekaa mkao wa kula kwa kushuhudia mashindano mbalimbali makubwa duniani kuanzia mwaka huu.
Mshikemshike wa mashindano hayo ulianzia jana Jumanne nchini India ambapo Kombe la Dunia la Wanawake waliochini ya miaka 17 linaanza. Timu ya Taifa ya Morocco inapambana na Brazil kuanzia saa 10.30 jioni na baadaye India itapambana na Marekani (The United States) kuanzia saa 2.00 usiku.
Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Serengeti Girls’ itashuka dimbani uwanjani leo Jumatano kupambana na Japan katika mchezo wa Kundi D kuanzia saa 11:30 jioni. Kabla ya mchezo huo, ratiba inaonyesha Canada itapambana na Ufaransa kuanzia saa 10.30 jioni.
Michuano hiyo itamalizika Oktoba 30. Baada ya mashindano hayo, mashabiki wa soka watapumua kwa siku 19 huku wakishuhudia michuano ya ligi mbalimbali kabla ya kushuhudia fainali za Kombe la Dunia yaliyopangwa kufanyika nchini Qatar.
Kuanzia Novemba 20, mashabiki wa soka watashuhudia mshike mshike wa michuano hiyo ambayo itamalizika Novemba 18.
Mashindano yote yatashuhudia matumizi makubwa ya Teknolojia ya Mwamuzi Msaidizi wa Video (VAR) ambapo kwa mara ya kwanza, Serengeti Girls watakuwa wanaitumia kwa mara ya kwanza.
Nimeanza kwa kuzungumzia mashindano mbalimbali (hasa ya Kombe la Dunia la India) kutokana na majukumu ya timu yetu ya taifa ya wanawake ambayo pia ndiyo mwakilishi pekee kwa nchi 16 za Kusini mwa Afrika (SADC) na Afrika Mashariki.
Ni wazi kuwa wachezaji wa Serengeti Girls watakuwa wa kwanza kuonja tamu na chungu ya VAR kwa upande wa timu ya taifa katika historia ya mpira wa miguu Tanzania.
Pamoja na ukweli kuwa kuna baadhi ya wachezaji wa Tanzania tayari wameonja maamuzi ya VAR katika mechi mbalimbali wakiwa na klabu zao, kwa timu ya Serengeti Girls inakuwa historia kwao kuonja maamuzi ya teknolojia hiyo.
Mashindano India yameingia katika historia kwani yanakuwa ya kwanza katika historia ya FIFA kwa mashindano maalumu ya umri kutumia teknolojia ya VAR.
Kwa mujibu wa Kari Seitz ambaye ni mkuu wa idara ya waamuzi wa kike wa FIFA wameamua kutumia teknolojia hiyo ili kupanua wigo na maendeleo ya soka kwa wadau hasa kwa kupitia maendeleo ya soka.
Seitz alisema kuwa teknolojia ya VAR itasaidia mchakato wa kufanya maamuzi sahihi kwa waamuzi na kuchangia kuleta haki katika mashindano hayo pamoja na kuwa na changamoto kadhaa.
Alisema kuwa changamoto zilizopo ni mwendelezo wa kujifunza na kuboresha zaidi teknolojia hiyo na bado wana wana nafasi ya kuendelea kutumia teknolojia hiyo.
Alifafanua juhudi zinafanyika ili kuondoa changamoto hizo na wanaamini baada ya muda mfupi, watafanikiwa na kuleta maendeleo makubwa sana katika mpira wa miguu.
Ni wazi VAR itajikita zaidi katika maamuzi ya mabao ya kufunga, rafu zenye maonyo au maamuzi ya kadi ya njano au nyekundu na penalti.
Kwa mujibu wa Seitz, timu ya VAR mara nyingi hufanya marejeo ili kubaini makosa ya wazi na dhahiri yanayohusiana na hali hizi nne za kubadilisha matokeo. Timu ya VAR huwasiliana na mwamuzi tu kwa makosa ya wazi na dhahiri au matukio makubwa ambayo hayakufanyika.
“Katika kuhakikisha kuwa mashindano ya wanawake ya U-17 yanafanikiwa kutakuwa moja ya mifumo mbalimbali ya kisasa ambayo itasaidia fainali za mashindano ya Dunia kwa timu za wakubwa ambayo yamepangwa kufanyika nchini Qatar Novemba mwaka huu,
Kombe la Dunia la Wanawake U-17 nchini India litakuwa mashindano ya tatu ya FIFA kwa wanawake kutumia VAR kufuatia Kombe la Dunia la Wanawake U-20 Costa Rica 2022 na Kombe la Dunia la FIFA la Wanawake Ufaransa 2019.
Hii itakuwa mara ya pili kwa teknolojia ya VAR kutumika nchini India, ya kwanza ikiwa ni kutoka hatua ya robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Asia la AFC ambalo nchi hiyo iliyofanyika Januari-Februari mwaka huu.
Wakati huohuo, Kamati ya Waamuzi ya FIFA pia ilitangaza wasimamizi wa mechi kwa ajili ya michuano hiyo inayojumuisha waamuzi 14 wanawake, waamuzi wasaidizi 28, waamuzi watatu wa ziada na waamuzi 16 wa VAR.
“Tunafuraha kwamba Kombe la Dunia la FIFA la Wanawake U-17 linarejea baada ya kusimama kwa miaka minne kulikosababishwa na janga la Uviko-19.
“Tunatarajia kuona mashindano mazuri, yenye msisimko na ushindani mkali huku waamuzi wakionyesha ubora wa hali ya juu,” alisema mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya FIFA Pierluigi Collina.
“Kwa wasimamizi wa mechi, bila shaka, ni hatua nyingine kubwa katika maandalizi ya waandaaji wajao wa michuano hiyo, Australia na New Zealand kwa mwaka ujao,” alisema.