Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serengeti Girls msiwaze ipo siku yenu

Serengeti Girls U17 Serengeti Girls msiwaze ipo siku yenu

Fri, 13 Sep 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Katika mashindano ya soka ya wanawake chini ya umri wa miaka 17 ya Umoja wa Vyama vya Mpira wa Miguu Kaskazini mwa Afrika (Unaf), timu ya taifa ya Tanzania ya umri huo imegawa sana dozi.

Ikiwa kama timu mwalikwa, imetwaa ubingwa wa mashindano hayo baada ya kukusanya pointi saba katika mechi tatu ilizocheza dhidi ya Misri, Morocco na Tunisia.

Katika mashindano hayo ya Unaf, Serengeti Girls ilianza kwa kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Misri, ikaifunga Morocco kwa mabao 5-3 na mechi ya mwisho ikatoka sare ya bila kufungana na wenyeji Tunisia.

Kutwaa ubingwa wa mashindano hayo tena bila kupoteza mechi hata moja dhidi ya Tunisia, Misri na Morocco ni jambo ambalo linapaswa kuifanya Serengeti Girls kupata pongezi na wapenzi na wadau wa soka hapa nchini.

Hizo ni nchi ambazo zimekuwa na uwekezaji mkubwa na usimamizi mzuri wa program za maendeleo ya mpira wa miguu ikiwemo soka la wanawake hivyo kupata matokeo mazuri dhidi yao sio kazi rahisi.

Nilitamani kuona Serengeti Girls nao wangeingizwa katika ule utaratibu wa kupata bonasi ya fedha za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kila bao ambalo linafungwa na timu ya Tanzania kwenye mashindano tofauti ambayo ni Sh5 milioni kwa kila bao linalofungwa.

Kwa mabao tisa ambayo imeyafunga huko Unaf maana yake ingepata kiasi cha Sh45 milioni, lakini pamoja na kutopata, tumefurahi kuona serikali ikitoa Sh30 milioni kwao.

Tunaamini fedha hizo Sh30 milioni zitawapa chachu na hamasa ya kufanya vizuri zaidi na ipo siku watapata nyingi pengine hata mara 10 ya hizo.

Chanzo: Mwanaspoti