Timu ya Taifa ya Wasichana wenye umri chini ya miaka 17 ‘Serengeti Girls’, itaiwakilisha nchi katika fainali za Kombe la Dunia zilizopangwa kufanyika India kuanza Oktoba 11 hadi 30 mwaka huu.
Tayari Serengeti Girls ipo Uingereza katika Mji wa Southampton kwa ajili ya kujiandaa na mashindano hayo. Kambi hiyo ni sehemu ya maandalizi ya mwisho ya timu hiyo kabla ya kutua India.
Mbali ya kuiwakilisha Tanzania, Serengeti Girls pia imeweka historia ya kuwa nchi ya kwanza kwa Ukanda wa Nchi za Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kufuzu katika mashindano hayo makubwa yanayosimamiwa na FIFA.
Ratiba inaonyesha Serengeti Girls itaanza kampeni ya kuwania ubingwa wa Kombe la Dunia dhidi ya Japan Oktoba 12 kwenye Uwanja wa Pandit Jawaharlal Nehru katika Mji wa Margao.
Mchezo huo wa Kundi D umepangwa kuanza saa 12.30 jioni kwa saa za Tanzania ambapo mechi ya ufunguzi katika kundi hilo itakuwa kati ya Canada na Ufaransa iliyopangwa kuanza saa 8.30 mchana kwa saa za Tanzania.
Mbali ya mechi hiyo ya kwanza Serengeti Girls itashuka uwanjani tena Oktoba 15 saa 8.30 mchana kwenye uwanja huohuo kabla ya kucheza mechi ya mwisho dhidi ya Canada kwenye Uwanja wa DY Patil kwenye Mji wa Navi, Mumbai ambapo siku hiyo, Ufaransa itashuka na Japan kwenye Uwanja wa Pandit Jawaharlal Nehru kwenye mji wa Margao. Advertisement
Nimeanza kwa kuzungumzia timu yetu ya Taifa ya Wasichana ya umri wa miaka 17 baada ya taarifa ya FIFA kuwa itatumia teknolojia ya mwamuzi msaidizi wa video maarufu kwa jina la VAR katika mashindano hayo.
Ni wazi kuwa wachezaji wa Serengeti Girls watakuwa wa kwanza kuonja tamu na chungu ya VAR kwa upande wa timu ya taifa katika historia ya mpira wa miguu Tanzania.
Ni wazi kuwa kuna baadhi ya wachezaji wa Tanzania tayari wameonja maamuzi ya VAR katika mechi mbalimbali wakiwa na klabu zao na wala si kwa timu ya taifa kama ilivyo kwa wachezaji wa Serengeti Girls.
Mashindano hayo yameingia katika historia kwani yanakuwa ya kwanza katika historia ya FIFA kwa mashindano maalum ya umri.
Kwa mujibu wa Kari Seitz ambaye ni mkuu wa idara ya waamuzi wa kike wa FIFA wameamua kutumia teknolojia hiyo ili kupanua wigo na maendeleo ya soka kwa wadau hasa kwa kupitia maendeleo ya soka.
Kwa mujibu wa Seitz, teknolojia ya VAR itasaidia mchakato wa kufanya maamuzi sahihi kwa waamuzi na kuchangia kuleta haki katika mchezo husika.
Alisema kuwa pamoja na changamoto kadhaa, bado wana nafasi ya kuendelea kutumia teknolojia hiyo huku wakifanyia maboreshi changamoto kadhaa.
Alifafanua kuwa kuna changamoto mbalimbali ya VAR, lakini juhudi zinafanyika ili kuondoa changamoto hizo na wanaamini baada ya muda mfupi, watafanikiwa na kuleta maendeleo makubwa sana katika mpira wa miguu.
Alisema kuwa ni wazi VAR itajikita zaidi katika maamuzi ya mabao ya kufunga, rafu zenye maonyo au maamuzi ya kadi ya njano au nyekundu na penalty.
Alisema kuwa timu ya VAR mara nyingi ufanya marejeo ili kubaini makosa ya wazi na dhahiri yanayohusiana na hali hizi nne za kubadilisha matokeo. Timu ya VAR huwasiliana na mwamuzi tu kwa makosa ya wazi na dhahiri au matukio makubwa ambayo hayakufanyika.
“Katika kuhakikisha kuwa mashindo ya wanawale ya U-17 atakuwa moja ya mifumo mbalimbali ya kisasa ambayo yatasaidia fainali za Kombe la Dunia kwa timu za wakubwa ambayo yamepangwa kufanyika nchini Qatar mwezi Novemba mwaka huu,
Kombe la Dunia la Wanawake U-17 nchini India litakuwa shindano la tatu ya FIFA kwa wanawake kutumia VAR kufuatia Kombe la Dunia la Wanawake U-20 Costa Rica 2022 na Kombe la Dunia la FIFA la Wanawake Ufaransa 2019.
Hii itakuwa mara ya pili kwa teknolojia ya VAR kutumika nchini India, ya kwanza ikiwa ni katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Asia la AFC ambalo nchi hiyo iliyofanyika Januari-Februari mwaka huu.
Kamati ya Waamuzi ya FIFA pia ilitangaza wasimamizi wa mechi kwa ajili ya michuano hiyo inayojumuisha waamuzi 14 wanawake, waamuzi wasaidizi 28, waamuzi watatu wa ziada na waamuzi 16 wa VAR.
“Tunafuraha kwamba Kombe la Dunia la FIFA la Wanawake U-17 linarejea baada ya kusimama kwa miaka minne kulikosababishwa na janga la Uviko-19.
“Tunatarajia kuona shindano zuri, lenye msisimko na ushindani mkali huku waamuzi wakionyesha ubora wa hali ya juu,” alisema mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya FIFA Pierluigi Collina.
“Kwa wasimamizi wa mechi, bila shaka, hii ni hatua nyingine kubwa ya maandalizi ya waandaaji wajao wa fainali hizo, Australia na New Zealand kwa mwaka ujao,” -alisema.