Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serengeti Girls itabebwa na haya

Sere U17.jpeg Wachezaji wa Timu ya Taifa ya wanawake U17 Serengeti Girls

Tue, 11 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Timu ya Taifa Tanzania ya Wanawake ya chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Girls tayari ipo India tayari kwa ushiriki wa Fainali za Kombe la Dunia zinazoanza leo nchini humo, huku yenyewe ikitarajiwa kutupa karata ya kwanza Jumatano dhidi ya Japan.

Michuano hiyo inayoshirikisha timu 16 kutoka mashirikisho ya soka sita tofauti wakiwamo watetezi Hispania, itafikia tamati Oktoba 30 baada ya kinyang’anyiro kitakachofanyika ndani ya miji mitatu ya nchini India zinakofanyikia fainali hizo za saba tangu ilipoasisiwa mwaka 2008.

Serengeti iliyokuwa imejichimbia kambini katika mji wa Southampton, Engand imepangwa Kundi D na timu za Japan, Ufaransa na Canada, huku Kundi A likiwa na timu za India, USA, Morocco na Brazili, Kundi B lina Ujerumani, Nigeria, Chile na New Zealand wakati Kundi C lina Hispania, China, Colombia na Mexico.

Timu hiyo ya Tanzania ambayo itamkosa mfungaji wake mahiri aliyetupia mabao 10 katika mechi za mchujo za fainali hizo kwa Afrika, Clara Luvanga ambaye hayupo katika kikosi cha wachezaji 21, itavaana na Japan keshokutwa kuanzia saa 11:30 jioni kwenye Uwanja wa Pandit Jawaharlal Nehru uliopo mji wa Margao, ukitanguliwa na mechi ya Canada na Ufaransa itakayopigwa saa 8:00 mchana.

Ratiba inaonyesha baada ya mechi hiyo ya Japan, Serengeti itashuka tena uwanjani Oktoba 15 saa 8.00 mchana kuikabili Ufaransa kwenye Uwanja wa Pandit Jawaharlal Nehru na kumaliza mechi za kundi hilo Oktoba 18 dhidi ya Canada kwenye Uwanja wa DY Patil kwenye Mji wa Navi, Mumbai.

Serengeti ipo kwenye Fainali za Kombe la Dunia huku wengi wakiwa hawaipi nafasi kubwa ya kutisha kwenye michuano hiyo kutokana na kutokuwa wazoefu kwani ni mara yao ya kwanza kushiriki. Licha ya kutopewa nafasi kubwa lakini Mwanaspoti linakuletea mambo yanayoweza kuibeba timu hiyo.

KAMBI YA ENGLAND

Kama kuna jambo ambalo litaibeba timu hii kwenye fainali hizi ni maandalizi yao iliyoyafanya hasa kuweka kambi ya wiki mbili nchini England.

Timu hiyo ilifikia mji wa Southampton ili kujiandaa na mashindano hayo na Ijumaa ilitua India tayari kwa fainali hizo za Kombe la Dunia.

Katika kambi hiyo Serengeti ilicheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Southampton ambapo mechi ya kwanza ilishinda mabao 3-0 na mechi nyingine ilitoka suluhu.

Kambi hiyo inaweza kuleta matunda mazuri kwa timu hiyo kwani imepata nafasi ya kufanya mazoezi yake kwa utulivu na pia mechi za kirafiki zimewapa mazoezi mazuri. Kocha Bakari Shime anasema wamepata wakati mzuri kwa kufanya mazoezi na kambi hiyo imetuliza akili za wachezaji wake.

“Tumekuwa na siku nzuri za mazoezi hapa (Engalnd), hali ya hewa ni mchanganyiko. Tumepata vitu vingi vizuri, akili za wachezaji zimechangamka kwani wameweza kupata mazingira tofauti na nyumbani Tanzania.

“Tumecheza mechi mbili za kirafiki zimetupa mazoezi mazuri na matumaini yangu siku ambazo tumekaa hapa zitakuwa zenye faida kwetu, licha ya kwamba malengo ya kiufundi tuliyokusudia hayakutimia lakini tumepata picha kwani tumecheza na timu ya Ulaya,” anasema Shime na kuongeza:

“Kwa bahati mbaya programu ya awali imekwenda tofauti kwani mwanzo tulipanga kukaa hapa England baadaye tuhamie Dubai kwa ajili ya michezo ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya timu za Taifa ambazo zingeenda kushiriki Kombe la Dunia, na tulipanga kupata timu tatu za mabara tofauti lakini imeshindikana.

“Safari ya kuja hapa Uingereza ilichelewa hivyo ikafinya nafasi ambayo kiufundi ingekuwa nzuri na kubwa kwangu kuona timu yangu inapata mechi nyingi za kirafiki na timu ambazo zinazoshiriki Kombe la Dunia.”

MASTAA WA VIWANGO

Licha ya mshtuko wa kutokuwepo kwa jina la Clara Luvanga aliyefunga mabao 10 kwenye mechi za mchujo, huku watu wengi kuonekana kutoipa nafasi kubwa ya kutikisa kwenye fainali hizo, bado inaweza kushangaza kutokana na uwepo wa wachezaji bora kwenye kikosi cha timu hiyo.

Uwepo wa wachezaji kama Aisha Juma, Noela Patrick, Husna Mtunda, Hasnath Linus, Joyce Lema, Christer Bahera na wengineo unaifanya kujiamini kutokana na ubora wa nyota hao. Clara ndiye aliibuka kinara wa ufungaji kwenye hatua ya kufuzu ushiriki wa fainali hizo baada ya kufunga mabao 10 na alishika nafasi ya pili duniani, lakini kukosekana kwake kunatarajiwa kuwa pengo.

WANAJIAMINI

Tanzania ni mara ya kwanza inashiriki fainali za Kombe la Dunia hivyo katika hali ya kawaida tu ni kwamba sio wazoefu kama ilivyo kwa mataifa mengine hasa ya Ulaya ambayo yamekuwa yakishiriki mara kwa mara wakiwemo mabingwa watetezi Hispania.

Hata hivyo, Serengeti itaingia katika michuano hiyo ikijiamini baada ya kupewa moyo na serikali na wadau wengi wa soka hapa nchini. Ni kama tu ilivyofanya Tembo Warriors iliyoshiriki Fainali za Kombe la Dunia kwa Walemavu na kushangaza dunia kwa kufika robo fainali ikiingia katika 8 Bora.

Baada tu ya kufuzu ushiriki wa fainali hizo, Serengeti ilialikwa Bungeni Juni 7 mwaka huu na kupongezwa na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia Julai 5 walialikwa Ikulu na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye aliwatia moyo na kuwataka kutoogopa bali wapambane kwani wanaweza.

“Serengeti Girls imeliheshimisha taifa letu, mmefanya jambo kubwa ambalo halijawahi kutokea nchini hata wanaume hawajawahi kushiriki Kombe la Dunia lakini ninyi mmethubutu na mmeweza, hivyo nendeni mkapambane kwenye mashindano hayo na mimi niko pamoja nanyi kuwasapoti,” alisema Rais Samia wakati akiipongeza timu hiyo.

WASIKIE WACHEZAJI

Nahodha wa Serengeti Girls, Noela Patrick anasema kila mchezaji ana kiu ya kucheza fainali hizo hivyo Watanzania wategemee mazuri kwani wataipambania nchi kwa muda wote. “Naamini kabisa tutafika mbali kwani kila mmoja wetu ana kiu ya kucheza na kuonyesha alichonacho na kupambania taifa letu.

“Kundi letu lina timu nzuri zenye wachezaji wazuri, wana uzoefu wa mashindano. Tunawaheshimu wapinzani wetu lakini hata sisi tumejiandaa na mpaka tumefika hapa inamaanisha pia na sisi ni wakubwa,” anasema Noela.

Kiungo Alihya Salum anasema hiyo ni fursa kubwa kwao kujitangaza hivyo lazima wajitoe kulipambania taifa.

“Kushiriki Kombe la Dunia ni levo ya mwisho kwa mchezaji kufikia hivyo ni fursa kubwa sana kwetu.Tunajua tunakutana na mataifa makubwa yaliowekeza kwenye mchezo huu lakini tuko tayari kwa mapambano,” anasema.

Kwa upande wa Rahma Hassan anasema; “Wote tuna morali, Watanzania wametutuma kazi hivyo lazima tupambane, hakuna kinachoshindikana na tunaweza kurudi na kombe Tanzania.”

Tanzania imefuzu Fainali za Kombe la Dunia kwa kuzifunga Botswana kwa jumla ya mabao 11-0, Burundi 4-1 na Cameroon 5-1 hivyo kuungana na timu nyuingine mbili kutoka Afrika ambazo ni Morocco na Nigeria.

Chanzo: Mwanaspoti