Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serengeti Girls, Canada ni heshima

Serengeti Girls X Canada Serengeti Girls, Canada ni heshima

Tue, 18 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Timu ya Taifa ya Wanawake chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Girls’, ina kibarua kizito leo Jumanne dhidi ya Canada kupigania nafasi ya kutinga robo fainali ya Kombe la Dunia linaloendelea kutimua vumbi nchini India.

Serengeti Girls ipo nafasi ya pili nyuma ya Japan kwenye msimamo wa Kundi D ikiwa na pointi tatu baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 kwenye mchezo uliopita dhidi ya Ufaransa.

Japan inaongoza kundi hilo kwa kuw na pointi sita baada ya kushinda michezo yake miwili dhidi ya Tanzania na Canada.

Kocha wa kikosi hicho, Bakari Shime alisema wachezaji wake wapo kwenye ari nzuri ya kimchezo baada ya kufanyia kazi mapungufu kadhaa ambayo yalijitokeza kwenye mchezo uliopita ni matarajio yao kufanya vizuri dhidi ya Canada na kutinga robo fainali.

“Kuna mapungufu ambayo tuliyaona kama benchi la ufundi kwenye mchezo wetu uliopita, tumejaribu kuyafanyia kazi ili kuwa bora zaidi kwenye mchezo wetu ujao ambao tunajua utakuwa mgumu,” alisema kocha huyo na kuendelea,

“Malengo yetu ni kufanya vizuri kadiri ambavyo itawezekana, wito wangu kwa Watanzania watuombee, naamini tunaweza kuvuka hatua ya makundi.”

Canada ndio timu inayoburuza mkia kwenye Kundi D ikiwa na pointi moja baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Ufaransna kwenye mchezo wao wa kwanza huku wakikumbana na kipigo dhidi ya vinara Japan cha mabao 4-0.

Wakati Serengeti Girls itakuwa ikicheza dhidi ya Canada, Japan yenyewe itakuwa ikikamilisha ratiba dhidi ya Ufaransa kwani wao tayari wamejikatia tiketi ya kutinga hatua ya robo fainali ambayo itaanza Oktoba 21.

Chanzo: Mwanaspoti