Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serengeti Boys yapewa mchongo kuiua Uganda kesho

52611 Pic+serengeti

Tue, 16 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati timu ya Taifa ya vijana, ‘Serengeti Boys’ ikitarajiwa kuvaana na Uganda, wadau wa soka wamempa mbinu Kocha Oscar Miramba wakimtaka kuboresha eneo la ulinzi.

Serengeti Boys ilianza vibaya Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon), baada ya kufungwa mabao 5-4 na Nigeria.

Timu hiyo kesho Jumatano itacheza mchezo wa pili dhidi ya Uganda ambayo juzi ilicharazwa bao 1-0 na Angola katika mechi ya usiku.

Kocha wa Prisons, Mohammed ‘Adolf’ Rishard alisema Serengeti Boys imeonyesha kiwango bora dhidi ya Nigeria, lakini Mirambo anatakiwa kuboresha safu ya ulinzi.

Rishard alisema safu ya ushambuliaji ya Serengeti Boys ilicheza vizuri, hivyo ina nafasi ya kuzifunga Uganda na Angola katika mechi zake.

"Washambuliaji wanafanya kazi wanafunga magoli, kinachotakiwa kuimarisha safu ya ulinzi ili timu inapofunga ihakikishe hayarudi, lakini si kwa kupaki basi," alisema Rishard.

Kocha wa Lipuli, Selemani Matola hakutofautiana na kauli ya Rishard kuhusu safu ya ulinzi akidai inatakiwa kupewa mbinu bora ya kujilinda katika mechi zote mbili zijazo.

"Mechi ilimalizika kwa mabao 4-5, ingawa ushindi ndiyo kila kitu, lakini wachezaji walipambana kilichopo ni kocha kuwarudisha mchezoni," alisema Matola.

Nahodha huyo wa zamani wa Simba, alisema kipa anatakiwa kupewa mbinu ya kuzungumza na mabeki wake muda wote wa mchezo.

Kwa upande wake kipa wa zamani wa Simba Idd Pazi alisema Serengeti Boys ina nafasi ya kusonga mbele katika fainali hizo kwa kuwa ina kikosi imara ambacho kinaweza kuzifunga Uganda na Angola.

Kauli ya Mirambo

Kocha wa Serengeti Boys, Mirambo alisema Uganda imeshika karata ya Tanzania katika fainali hizo, hivyo watacheza kufa au kupona kupata ushindi kesho.

"Tumefungwa mechi moja, lakini hatujatolewa katika mashindano. Mechi dhidi ya Uganda ni tofauti, ndiyo itaturejesha katika ramani. Bahati tumewasoma Uganda uchezaji wao," alisema Mirambo.

Alisema katika mazoezi benchi la ufundi linafanyia kazi matumizi ya nguvu kwa kuwa Uganda inacheza soka ya kutumia nguvu.

Timu mbili za juu Kundi A na B zitakata tiketi ya kuwakilisha Afrika katika Fainali za Kombe la Dunia zilizopangwa kufanyika Brazil.



Chanzo: mwananchi.co.tz