Ofisa Mtendaji Mkuu wa zamani wa Yanga, Msauzi, Senzo Mazingiza amekuwa akiifuatilia timu hiyo kwa karibu ikiwamo kuitazama mechi iliyopita dhidi ya Al Hilal ya Sudan na amewashusha presha mashabiki wenzake akiwaambia wasiisakame timu kama vile imepoteza baada ya sare ya 1-1, akisema bado ina nafasi kwa mchezo wa marudiano utakapigwa Jumapili jijini Khartoum, Sudan.
Kisha akamgeukia Nabi na kumwambia ili atoboe ugenini ni lazima akipangue aua kurekebisha kikosi chake hasa eneo la ulinzi na kiungo akisema lazima wawepo watu wagumu wa kuzuia na kasi katikati.
“Nafikiri ni mechi ambayo kocha wetu (Nabi) anatakiwa kubadilisha eneo la ulinzi hatukuwa wagumu kama ambavyo tulitakiwa kuwa, lakini hata eneo la kiungo hasa katikati nako kunahitajika mabadiliko makubwa,” alisema Senzo ambaye amewaachia Yanga mataji matatu msimu uliopita na kuongeza;
“Unajua mechi ya kwanza tulicheza vizuri nashangaa kwanini watu wanaona kama Yanga imefanya vibaya sana, tunatakiwa kuiheshimu Al Hilal, kitu bora ni kwamba kuelekea mechi ijayo vijana wetu kule mbele wanahitaji kutulia kutumia nafasi.”
Katika mechi ya kwanza iliyopigwa wikiendi iliyopita, ukuta wa Yanga uliundwa na kipa Diarra Djigui, Djuma Shaban, Shomary Kibwana, Dickson Job na Yannick Bangala, huku viungo wakiwani Khalid Aucho na Feisal Salum, huku mbele kukiwa na Jesus Moloko, Fiston Mayele, Aziz KI na Bernard Morrison na Senzo alisema eneo la mbele lilijitahidi sambamba na kipa Diarra aliyeokoa timu isizame.
“Nampongeza sana Morrison (Bernard) alifanya vizuri sana, Mayele (Fiston) alifunga sawa, lakini anahitajika kuwa mtulivu kutumia nafasi zaidi, Aziz (KI) naye huu ni wakati kutuonyesha kile bora kutoka kwake namjua anaweza kuwa na mabadiliko makubwa kama atapewa nafasi,” alisema Senzo.
Senzo ameshauri pia kwa kutaka wachezaji wapewe motisha kubwa itakayowajaza ujasiri wa kupigana kuzuia presha ya Al Hilal wakiwa nyumbani, kwani rekodi zinaonyesha Al Hilal wakiwa kwao huwa na mzuka mwingi.
“Namwamini Nabi anajua kuzungumza kisaikolojia vizuri na wachezaji, lakini viongozi nao kuna namna wanaweza kuboresha morali kwa wachezaji kabla ya mechi, kuna kitu kikubwa wanatakiwa wapewe ikiwamo maneno mazuri na ahadi kubwa vitakavyowaogezea nguvu zaidi,” alisema.
Aidha bosi huyo ametamani kuona Afisa Mtendaji Mkuu wa timu hiyo Andre Mtine naye akiwahi mapema nchini humo kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa kabla ya timu kufika akitumia uzoefu wake.
“Najua kuna mtu atakuwa ameshatangulia kule kutoka Yanga lakini ningefurahi kama Andre (Mtine) naye akiwahi kule haraka, namfahamu ni mtu ambaye anajua mazingora ya siasa za soka za Afrika, ndio maana Yanga ikamchukua, kuna mambo mengi ya akili kubwa yatakiwa kupangwa vyema kule kabla ya timu kufika ili yasiharibu utulivu wa kikosi,”ambaye aliwahi kuwa Mtendaji mkuu wa Simba kabla ya kuhamia Jangwani.