Timu ya Senegal imefanikiwa kutwaa Kombe la Matafa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Morocco Uwanja wa Nelson Mandela Jijini Algiers.
Haukuwa ushindi mwepesi, kwani Simba Wadogo wa Teranga ilibidi watoke nyuma baada ya kutanguliwa kwa bao la Nahodha wa Morocco, Abdelhamid Ait Boudlal dakika ya14, kabla ya Serigne Falou Diouf kusawazisha kwa penalti ya msaada wa VAR dakika ya 79.
Shujaa wa Senegal alikuwa ni Mamadou Sawane aliyefunga bao la ushindi dakika ya 83 kuipa nchi yake taji la kwanza kabisa la AFCON U17, ambalo linakuwa la tatu kwa Taifa hilo ndani ya miezi minne baada ya awali kubeba mataji ya CHAN mwezi February huko huko Algeria na AFCON U20 mwezi Machi nchini Misri.
Ikumbukwe kampeni hii ya kukusanya mataji ilianzishwa na timu yao ya taifa ya wakubwa, baada ya kubeba taji la AFCON February mwaka jana na baadaye mwaka huo wakachukua na AFCON ya Beach Soccer.