Kocha Msaidizi wa Simba SC Seleman Matola Seleman Matola amesema msimu wa 2021/22, umemalizika salama wa salmini, huku kila mchezaji wa klabu hiyo akipata nafasi ya kuitumikia klabu hiyo.
Simba SC imemaliza msimu wa 2021/22, ikiwa nafasi ya pili katika Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kutolewa hatua ya Nusu Fainali Kombe la Shirikisho ‘ASFC’, huku wakipoteza mataji yote.
Kocha Matola ambaye alikabidhiwa jukumu la kukaimu nafasi ya Kocha Mkuu baada ya kuondoka kwa Kocha Franco Pablo Martin, amesema wachezaji wote walionyesha uwezo, japo hawakufikia lengo la kutetea mataji.
Amesema katika michezo mitano ya mwisho aliyosimama kama Kaimu Kocha Mkuu wachezaji wote walionyesha uwezo mkubwa wa kupambana.
“Kuhusu wachezaji wote wameonyesha kiwango bora katika michezo hii mitano ya mwisho”
“Kuhusu ni nani anakuja kuelekea msimu ujao nadhani tayari ripoti ya usajili ipo kwa kamati ya usajili tayari”
“Tumetoka kumaliza msimu kwa hiyo baada ya wiki moja kila kitu kitakuwa wazi” amesema Matola
Tayari Simba SC imeshamtangaza Kocha Mkuu mpya Zoran Maki ambaye atafanya kazi kwa kusaidizana na Kocha Mzawa Matola kuanzia msimu ujao wa Ligi Kuu na Michuano ya Kimataifa, inayoratibiwa na Shirikisho la soka Barani Afrika CAF.