Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sekondari mpya kupunguza mimba, utoro

TTHUB Mimba Sekondari mpya kupunguza mimba, utoro

Tue, 13 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Changamoto ya wanafunzi kutembea umbali wa zaidi ya kilomita nane hadi 10 kwenda Shule ya Sekondari Bulyanhulu imepatiwa ufumbuzi baada ya kujengwa shule mpya katika kijiji cha Busulwangili.

Mradi huo ni utekelezaji wa miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) katika vijiji vinavyopakana na mgodi wa Barrick Bulyanhulu.

Baadhi ya wakazi wa Kata ya Bulyanhulu waliozungumza na Mwananchi mwishoni mwa wiki walisema utekelezaji wa mradi huo si tu umewapunguzia wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu, bali pia utapunguza tatizo la utoro na mimba miongoni mwa wanafunzi wa kike waliokuwa wakikumbana na vishawishi vya madereva bodaboda waliokuwa wakiwarubini kwa lifti.

Charles Maduhu, mkazi wa kijiji cha Busulwangili alisema licha ya kuwajengewa shule pia mgodi huo unaendelea kuwajengea uzio utakaowasaidia wanafunzi kusoma kwa utulivu.

Rahima Nkuba, mkazi wa kijiji cha Busulwangili alisema, “Tunaushukuru uongozi wa mgodi wa Barrick Bulyanhulu kwa kushirikiana na Serikali na kutumia sehemu ya mapato yao kusaidia miradi mbalimbali ya kijamii ukiwepo mradi huu wa shule ya wasichana wenye vipaji maalumu."

Kwa upande wake, kaimu meneja wa mahusiano ya jamii wa mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Zuwena Senkondo alisema kumekuwa na changamoto ya mimba za utotoni, watoto wa kike kufanyiwa ukatili wa kubakwa wakiwa wanakwenda shule, hivyo mgodi ukaamua kutoa Sh800 milioni kwa ajili ya kuwajengea shule hiyo, ili kutokomeza mimba za utotoni.

"Pia shule hii itasaidia kuondokana na changamoto za ukatili na miradi hii tunaifanya kwa kushirikiana na Halmashauri ya Msalala kupitia fedha ya jamii ya CSR,"alisema Senkondo.

MsimaMizi wa mradi wa ujenzi wa shule ya wasichana Bulyanhulu, James Mukasa alisema ujio wa shule hiyo utaondoa changamoto nyingi, kwani kulikuwa na msongamano wa wanafunzi katika shule mama iliyopo ilikuwa na wanafunzi 2700, lakini kwa sasa watapungua, hivyo watasoma kwa uhuru hawatabanana tena.

"Shule hii tayari imekamilika kwa asilimia 99 ambayo ina vyumba 12 vya madarasa viti 320 na meza 320, kuna jengo la utawala, maabara, vyoo vimekamilika na vyumba vya bweni vipo 20 ambapo kila chumba watalala wanafunzi wanne, hivyo kufikia Julai majengo yote yatakuwa yamekamilika," alisema Mukasa.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Msalala, Charles Fusi alisema watoto wa kike walikuwa wakitembea umbali mkubwa, hivyo mgodi ukaona uwaokoe kwa kupitia fedha za CSR, ili waweze kutimiza ndoto zao.

“Niwaombe wazazi waendelee kuwa na uhusiano mzuri na mgodi, ili uendelee kutoa misaada mbalimbali katika jamii,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live