Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Second chance; Samatta aachiwa msala KRC Genk

Mbwana Samatta Mbwana Samatta

Tue, 7 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mshambuliaji wa Kinigeria mwenye urefu wa futi sita na inchi saba,Paul Onuachu alikuwa mmoja wa wachezaji wawili ambao walisajiliwa na watakatifu, Southampton dakika za mwisho wakati wa usajili wa dirisha dogo na kumwachia msala nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta kwenye kikosi cha KRC Genk huko Ubelgiji.

Januari 20, 2020, Samatta alimwachia msala Onuachu ambaye wakati huo akiwa mgeni kwenye klabu hiyo, nahodha huyo wa Taifa Stars alitia saini kwenye karatasi za mkataba wa miaka minne na nusu kujiunga na Aston Villa ya Ligi Kuu England.

Onuachu alikipokea kijiti kutoka kwa Samatta na kuwa mmoja wa washambuliaji hatari huko Ubelgiji takwimu zake zinatisha kwani kwenye michezo 114 (2019ñ2023) alipachika mabao 74, yakiwemo 21 ya msimu uliopita ambapo alishika nafasi ya tatu kwenye vita ya ufungaji bora kwenye ligi, kinara alikuwa Mjerumani, Deniz Undav wa Union St. Gilloise aliyepachika mabao 26.

Licha ya Samatta kuweka rekodi kadhaa akiwa na Aston Villa mambo hayakumnyookea akajikuta akitua Fenerbahce ambako na kwenyewe hakuwa na wakati mzuri na badala yake akajikuta akirejea Ubelgiji kwa mara ya tatu, ya pili ikiwa kwa mkopo.

Awamu yake ya pili na ya kwanza kukopeshwa baada ya kuwa mchezaji wa Fenerbahce ilikuwa kuichezea Royal Antwerp na sasa ni KRC Genk ambako alimkuta Onuachu ambaye gari lilikuwa limewaka na hatimaye kusugua benchi.

Pamoja na kwamba Samatta aliondoka Genk kipindi kile jina lake likiimbwa kila kona kutokana na makubwa ambayo alifanya ikiwemo kuipa ubingwa timu hiyo msimu wa 2018/2019 huku akifunga mabao 23 hakuwa akipata nafasi mbele ya mshambuliaji huyo.

MSALA WENYEWE

Kuondoka kwa Onuachu kunamaana kuwa Samatta ndiye anayetegemewa kwa sasa na KRC Genk kuongoza mashambulizi ya timu hiyo hivyo atakuwa na nafasi ya kurejea kwenye makali yake kutokana na nafasi ambayo atakuwa akipata mara kwa mara.

Kutokana na ufinyu wa nafasi msimu huu, Samatta alijikuta akicheza kwa dakika 464 badala ya 1530 kama angekuwa chaguo la kwanza. Amepachika bao moja tu.

Onuachu ameondoka na kuiacha KRC Genk ikiwa nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi Kuu Ubelgiji ‘Jupiler Pro’ ikiwa na pointi 59 kabla ya mechi za jana, Jumapili kwenye michezo 23 wapo juu kwa tofauti ya pointi sita huku akiwa kinara wa mabao akipachika 15, hivyo kwa Samatta kazi ni kwake.

KRC Genk ni miongoni mwa timu ambazo huwa zinafanya biashara kubwa kwenye soka la Ulaya kutokana na utamaduni ambao wapo nao wa kununua wachezaji wa bei chee wengine wanawazalisha wenyewe na baadae kuwauza.

kwenye dili ya Onuachu imepiga Pauni 18.5milion ambazo ni zaidi ya Sh. 500milioni. Nyota wengine ambao wamepita KRC Genk kwa vipindi tofauti na wanafanya makubwa Ulaya ni pamoja na Kelvin De Bruyne na Leandro Trossard ambaye yupo Arsenal huyu alicheza kikosi kimoja na Samatta kipindi hicho akiwa wamoto.

NAFASI YA KUSAJILIWA

Kama Samatta atafanya vizuri kwenye awamu yake hii ya pili kuichezea KRC Genk kwa kipindi ambacho kimesalia anaweza kuwa kwenye nafasi nzuri ya kusajiliwa moja kwa moja kwenye klabu hiyo kutokana na klabu yake ya Fenerbahce kumweka sokoni.

Fenerbahce inaonekana kutokuwa na mipango na Samatta ambaye mkataba wake na wababe hao wa soka la Uturuki unatarajiwa kumalizika Juni 30, 2024.

Wiki chache zilizopita Samatta alikuwa akihusishwa na miamba ya soka la Afrika, Al Ahly ambao wanahitaji huduma ya mshambuliaji wa kati kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia upande wa klabu, lakini kuondoka kwa Onuachu kunaweza kuzima hilo.

Chanzo: Mwanaspoti