Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sebusebu , kipa wa Geita Gold aliyeanza kama kiungo

Kipa Wa Geita Pic Sebusebu , kipa wa Geita Gold aliyeanza kama kiungo

Fri, 16 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Novemba, mwaka huu umekuwa mwezi wenye misukosuko kwa kipa wa Geita Gold, Sebusebu Samson baada ya kuzuka sakata la nyota saba wa klabu hiyo kutoweka kambini kutokana na maelewano mabovu na uongozi wakishinikiza kulipwa stahiki zao ikiwamo mishahara.

Baadhi ya nyota waliotajwa kutoweka kambini walikuwa ni Saido Ntibazonkiza, George Mpole, Ramadhan Chombo ‘Redondo’, Oscar Masai, Hussein Bakari na Sebusebu Samson, taarifa ambazo ziliifikia familia ya kipa huyo na kupigiwa simu nyingi na ndugu huku wakimshangaa na kumfokea wakidhani amegeuka na kupoteza mwelekeo.

Sebusebu anasimulia kwamba baada ya kuzuka taarifa hizo ndugu walimtukana na kumhoji kwanini ameacha kupigania ndoto zake. Anasema jambo hilo lilimshangaza na kumvuruga kwani hazikuwa taarifa za kweli na zilimuumiza huku wachezaji wenzake kambini wakimtania kuwa wanakaa na mzimu wake.

Katika mahojiano yake na Mwanaspoti, anasema yeye na wanaotajwa kugoma (Saido, Oscar Masai, Hussein Bakari na Ramadhan Chombo) walikuwepo kambini na siku hiyo walikuwa wametoka mazoezini, ambapo anasisitiza katika maisha yake ya soka hajawahi kukosa programu za mazoezini hata awe anaumwa lazima afike akae jukwaani atazame wanachofanya wenzake.

“Nilikuwa kambini nimelala baada ya kutoka mazoezini, mchana nikapokea simu ya dada akinitukana nikamuuliza kuna nini, akasema nimeanza kufanya ujinga, nimetoroka kambini, alinihoji sana akauliza niko wapi, nikamjibu niko kambini na simu yake ndiyo imenishtua nimetoka mazoezini akashangaa.

“Akaniambia niwashe data, usingizi ukakata, akanitumia baadhi ya taarifa hizo lakini nilimtoa wasiwasi. Ilibidi nijieleze sana kwani hakuamini, alikuwa sahihi kunipigia simu na kunifokea kwa sababu ameshanishauri sana. Baadaye nikapigiwa na kaka, nikamtuliza kwakuwa hazikuwa taarifa za kweli.”

Anasema baada ya kuona anapigiwa sana alimtafuta Oscar Masai kumuuliza kulikoni ambapo naye alimjibu kuwa ameona taarifa hizo na kumshauri aachane nazo kwani ni kawaida baadhi ya watu huzusha mambo.

“Kesho yake mazoezini wenzangu wakawa wananitania kwamba ni mimi au mzimu wangu na kushangaa tumeshinda wote mazoezini lakini taarifa zinasema sipo kambini. Nilishangazwa na kuumizwa na taarifa hizi. Ni jambo ambalo sikuwahi kukutana nalo, habari hizi zinaweza kumharibia mtu na kumtoa kwenye njia,” anasema Sebusebu.

ALIPOANZIA SOKA

Sebusebu ni mzaliwa wa Buchosa wilayani Sengerema, Mwanza ambaye kipaji chake kilianza kuonekana akiwa shule ya msingi akicheza nafasi ya kiungo mkabaji (namba sita). Licha ya baba yake kupinga vikali yeye kucheza soka baada ya kaka yake kuvunjika mkono kwenye moja ya mechi, lakini kipaji chake kiliendelea kukua na kupata umaarufu kitaani.

“Nilipofika kidato cha kwanza baba alifariki na hapo ndipo nilipopata uhuru zaidi wa kucheza soka kwa sababu mama alikuwa hana tatizo mimi kucheza, aliniambia nifanye kilicho sahihi lakini nisivunje sheria za Mungu na za serikali,” anasema.

Anasema safari yake ya kuwa kipa ilianza akiwa kidato cha kwanza baada ya kipa wa darasa lao kugoma ndipo akapewa nafasi na kudaka penalti mbili, nyota ikazidi kukua na kuwa kipa wa shule yao, timu ya mtaa hadi ya kanda na kuibukia Buseresere FC ya Geita kwenye Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL).

Akajiunga na Kabela City ya Kahama na kushiriki Ligi ya Mabingwa wa Mikoa mkoani Kagera ambapo aliyekuwa kocha wa Toto Africans, Almas Moshi alimkubali na kumchukua akakipiga Ligi Daraja la Kwanza (sasa Championship) msimu wa mwaka 2017/2018.

Msimu wa mwaka 2018/2019 alijiunga na Pamba ya Mwanza Daraja la Kwanza na kucheza playoff dhidi ya Kagera Sugar kusaka nafasi ya kwenda Ligi Kuu lakini wakatolewa kwa mabao 2-0. Msimu uliofuata akajiunga na Geita Gold na kuiwezesha kupanda Ligi Kuu akiwa langoni katika mchezo wa mwisho wakishinda 2-0 mbele ya Fountain Gate.

“Nashukuru watu ambao nimekuwa nao wamenipa ushauri wamenijenga na kujiamini, msimu huu tumeshiriki mashi-ndano ya kimataifa, nimepata nafasi ya kucheza mechi yangu ya kwanza ya kimataifa. Ni kitu kikubwa kwangu natamani kiwe na mwendelezo nifike hatua fulani niwe nacheza mechi hizo kila mara,” anasema kipa huyo.

AJIVUNIA SOKA

Kipa huyo anasema soka limebadili historia yake kwani anajivunia mengi ambayo ameyavuna kwenye mchezo wa huo ikiwemo uzoefu, mbinu, mafanikio katika maisha na kutengeneza marafiki wengi huku akiapa kuendelea kupambana kwa ajili ya familia na ndugu zake.

“Soka limebadili kwa kiasi kikubwa maisha yangu ni kitu ninachokitegemea kwa sasa kuendesha maisha yangu, ninaifanya kazi hii kwa ajili ya familia na ndugu zangu, naitegemea na ndiyo umenifikisha hapa, naendelea kupambana nifike mbali zaidi,” anasema

Anasema ni bahati kucheza Geita Gold sambamba na wachezaji wakubwa na wazoefu kama Kelvin Yondani, Juma Nyoso na makipa Benedict Tinoco, Abubakar Khomeiny na Aaron Kalambo ambao wamemsaidia kukua, kujifunza, kuimarika na kuwa kipa bora.

“Mechi yangu ya kwanza Ligi Kuu ilikuwa ugenini dhidi ya Mbeya City nikapata ‘cleansheet’ na nilicheza vizuri. Kilichonisaidia nilikuwa najifunza sana kutoka kwao wakati wa mechi na mazoezini walikuwa wananikubali na nikipewa nafasi walikuwa hawana wasiwasi, naweza kusema ndiyo kitu kikubwa kimenisaidia kufika hapa,” anasema.

KILICHOMPELEKA KWENYE SOKA

Anasema kilichomvutia kuingia mazima kwenye soka ni baada ya kufeli kidato cha nne ndio akaamua kuwekeza kwenye kipaji chake cha kusakata kabumbu huku akimtaja kipa mkongwe, Juma Kaseja kuwa ni nyota aliyemvutia kuupenda mchezo huo.

“Baada ya kufeli shule nikaona nikomalie kipaji changu nikipambanie nione Mungu atanifikisha wapi, nashukuru sasa niko hapa. Napambana nipige hatua zaidi. Sehemu ya malengo imeshatimia lakini bado nina njaa ya mafanikio,” anasema.

NJE YA SOKA

Samson anasema kama asingekuwa mwanasoka basi angekuwa mfanyabiashara kwa sababu ni fani anayoipenda huku muziki ukiwa sehemu kubwa ya maisha yake akiwa nje ya majukumu yake ya mpira.

“Nje ya mpira napenda sana kufanya biashara ndiyo kazi inayonivutia niwe na vitu vyangu vinavyoniingizia fedha. Nikiwa likizo kabla sijafanya lolote nahakikisha napata muda wa kukaa na mama yangu hata siku tatu, nikiwa kwangu napenda kusikiliza muziki, kucheza game (PS), kukaa na marafiki na kupika,” anasema

SALUTI KWA KASEJA

Anasema kipa wake bora wa muda wote nchini ni Juma Kaseja ambaye siku zote anatamani kucheza naye kwani anamvutia namna anavyosimama langoni, kuanzisha mipira na mashambulizi na nje ya Tanzania anavutiwa zaidi na kipa wa timu ya taifa ya Cameroon, Andre Onana.

Anataja makipa wake bora watano nchini kuwa ni Juma Kaseja, Deogratias Munishi, Aishi Manula, Metacha Mnata na yeye mwenyewe (Sebusebu Samson) huku akivutiwa na ushindani uliopo kwa sasa nchini kwa makipa wa timu za Ligi Kuu.

Chanzo: Mwanaspoti