Uongozi wa Simba SC unaendelea na mkakati wa kumalizana na kiungo mkabaji kutoka Burkina Faso, Ismail Sawadogo, baada ya kugoma kutolewa kwa mkopo.
Majuma mawili yaliyopita Uongozi wa Simba SC ulikutana Sawadogo kutaka kumvunjia mkataba, lakini Kiungo huyo aligoma na kutaka alipwe zaidi ya Milioni 700 ambazo klabu hiyo haiku tayari kumlipa.
Jambo hilo, limekuwa gumu na kusababisha SimbaSC kutaka kumtoa kwa mkopo mchezaji huyo kwenda timu nyingine, hali ambayo inaendelea kuwakutanisha Viongozi wa juu wa klabu hiyo kika kukicha ili kupata ufumbuzi.
Taarifa kutoka ndani ya Simba SC, zinadai kuwa nyota huyo amegoma kuondoka kwa mkopo, anachotaka yeye ni kuuzwa au kuvunjiwa mkataba wake wa miaka miwili ambao alisaini mwezi Januari 2023, mkataba wa miaka miwili.
“Mchezaji sasa yupo nyumbani kwao, kama ikitokea kuna timu itataka kumnunua mchezaji atauzwa kwa zaidi ya sh. bilioni moja, hivyo hataki kuondoka bure na huo ndiyo msimamo wake,” imeeleza taarifa hiyo.
Meneja wa Habari na Mawasiliano ya Simba, Ahmed Ally, amesema uongozi upo katika maboresha kikosi, kila mchezaji ambaye atatakiwa kubaki atabaki na atakayetakiwa kuondoka ataondoka, hakuna kinachoshindikana.
“Tunafuata maelekezo ya Kocha Roberto Oliviera ‘Robertinho’, yeye ndiye mwamuzi wa mwisho kama akisema mchezaji hayupo katika mipango yake, uongozi utalazimika kuachana naye kwa namna yoyote,” amesema.
Sawadogo aliyesajiliwa katika dirisha dogo, aliwahi kuzichezea klabu za ENPPI ya Misri, US Ouagadougou, Al-Arabi SC ya Kuwait na El Jadida ya Morroco.
Hadi sasa, Simba SC imeshaachana na nyota watatu wa kigeni ambao ni Mohamed Ouattara, Nelson Okwa na Victor Akpan.
Wachezaji wa kigeni waliopo Simba SC ni Sawadogo, Henock Inonga, Moses Phiri, Joash Onyango, Said Ntibazonkiza, Clatous Chama, Jean Baleke, Pape Sakho, Augustine Okrah na Peter Banda.
Wazawa walioagwa Simba SC ni Beno Kakolanya, Jonas Mkude, Erasto Nyoni na Gadiel Michael.