Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sasa ndo mtaona!

SIMBA BALEKE AD.jpeg Mastaa wa Simba

Sun, 22 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Simba inawakosa nyota 10 akiwamo Clatous Chama leo wakati itakapokabiliana na Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma kuanzia saa 1:00 usiku, lakini benchi lake la ufundi chini ya Robertinho Olivieira limeonekana halina hofu juu ya hilo.

Na kubwa zaidi limewataka mashabiki wajitokeze kwa wingi uwanjani hapo kuona vifaa vitatu vipya walivyovinasa katika dirisha dogo la usajili, washambuliaji Mohamed Mussa na Jean Baleke pamoja na kiungo Ismail Sawadogo.

Kocha msaidizi Juma Mgunda alisema nyota hao wapya wa Simba, wako tayari kwa kazi na Mungu akipenda, wote wataonekana uwanjani leo kushiriki katika kupigania ushindi na pointi tatu dhidi ya wabishi wa Dodoma Jiji.

"Ni usajili wa dirisha dogo. Mtu anasajiliwa ambaye yuko tayari. Haji kutayarishwa. Wachezaji ambao tumewasajili, wako tayari na Inshallah kwa uwezo wa Mungu wataonekana," alisisitiza Mgunda.

Dodoma Jiji wamekuwa na mwendo wa kusuasua kwenye Ligi Kuu msimu huu na mechi 10 zilizopita zinaweza kuonyesha uhalisia wa hilo ambapo wamepata ushindi mara tano na kupoteza michezo mitano.

Wenyeji katika mchezo wa leo wanapaswa kuwa makini zaidi katika safu yao ya ulinzi ambayo imeruhusu mabao 25, kwani wanakutana na Simba yenye safu tishio ya ushambuliaji msimu huu ambayo hadi sasa imepachika jumla ya mabao 50, huku katika mechi 10 zilizopita ikipachika mabao 31 sawa na wastani wa mabao 3 kwa kila mechi.

Na benchi la Dodoma Jiji linaonekana kulifahamu hilo kwa kukiri hadharani kuwa wanatakiwa kufanya kazi ya ziada ili kuvuna pointi tatu dhidi ya Simba leo.

"Simba ni moja kati ya timu bora sana Afrika. Tutakutana na mechi ngumu lakini sisi kama Dodoma Jiji tumejipanga kukabiliana nao. Nichukue nafasi hii kuwaambia mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi ili tujisikie tupo nyumbani wakitusapoti," alisema kocha msaidizi wa Dodoma Jiji, Kassim Liogope.

Dodoma Jiji wamekuwa sio tishio wanapocheza nyumbani na hasa dhidi ya Simba hivyo hapana shaka mchezo wa leo kwa maana nyingine ni fursa kwao kukataa unyonge.

Takwimu zinaonyesha katika mechi 10 za ligi zilizopita ambazo Dodoma Jiji wamecheza wakiwa nyumbani, wamepata ushindi mara nne tu na kupoteza michezo sita huku wakifunga mabao nane na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara 11.

Wapinzani wao leo, Simba wamekuwa na takwimu nzuri ugenini na kuthibitisha hilo, katika mechi 10 zilizopita za ligi ambazo wamecheza wakiwa hawapo nyumbani, wamepata ushindi mara tano, kutoka sare nne na kupoteza mchezo mmoja, wakifunga mabao 22 huku wenyewe wakifungwa mabao saba.

Tangu Dodoma Jiji ipande Ligi Kuu, imecheza mechi tano dhidi ya Simba ambazo zote imepoteza, ikifunga mabao mawili tu huku yenyewe ikifungwa mabao 11.

Simba katika mechi ya leo itawakosa wachezaji 10 tofauti kutokana na sababu mbalimbali ambapo Mzamiru Yassin, Pape Sakho, Joash Onyango na Sadio Kanoute hawatocheza kwa vile wanatumikia adhabu ya kukosa mchezo mmoja baada ya kukusanya kadi tatu za njano, lakini pia watamkosa Chama anayedaiwa kuwa mgonjwa.

Wengine ni Jonas Mkude ambaye hajasafiri na timu huku sababu ikiwa haijawekwa wazi, Peter Banda na Israel Mwenda ambao bado hawajawa fiti pamoja na majeruhi, Moses Phiri na Enock Inonga.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live