Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sare ya Brazil yazusha balaa

Brazil Sdn Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Brazil

Sat, 3 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Karibu kila rangi imepewa tafsiri yake. Kwa mfano nyeusi na zambarau ni kwa msiba, hofu, maafa na mambo ya huzuni. Rangi ya njano ambayo ni ya jua inawakilisha raha na furaja, ujana na uchangamfu. Kwa watu wa Brazil manjano ni rangi inayopendwa zaidi kuliko nyengine na ukichunguza utaona popote pemnye mkusanyiko wa watu basi wengi huwa na vazi la rangi ya kijano.

Watu wa Brazil wanaiona rangi ya njano kuwa ni ya kheri na baraka na yenye kuleta mafanikio na faraja na siku hizi wapo ambao huwa hawafurahii wanapoona timu yao ya taifa imevaa jezi rangi nyengine na sio ya njano.

Mara kadha timu hio imewahi kukataa kucheza mashindano ya Amerika ya Kusini ilipotakiwa kuvaa jezi ambayo si ya rangi ya njano. Mpaka katika miaka ya 1950 Timu ya Brazil ilitumia sare ya rangi nyeupe na buluu.

Lakini baada ya kukosa Kombe la Dunia katika uwanja wa nyumbani kwa kufungwa na Uruguay 2-1 baada ya kuongoza 1-0 mpaka dakika za mwisho pakazuka zahma baada ya waganga kusema rangi hizo zilikuwa na mkosi na timu ya Brazil.

Baada ya majadiliano marefu na kuchukuliwa maoni nchi nzima iliamuliwa kutumia rangi ya njano ambayo ndio inayopendwa sana na watu wa nchi hio na hata kutumika kwa bendera ya taifa ya nchi hio.

Kwa bahati nzuri tokea kubadili rangi ya sare ya timu ya taifa, Brazil ilipata mafanikio makubwa na kuwa na wachezaji kama Pele, Jairzinho, Tostaio, Rivelino, Zitto na hivi karibuni akina Ronaldo. Timu ya Brazil ilitajika kuwa timu bora duniani mpaka mwanzoni wa karne ya 21.

Sasa pamezuka zogo jipya baada ya Brazil kutofanya vizuri katika soka kama ilivyokuwa miaka iliopita. Nalo la kutaka kuachana na sare ya njano na mara chache Brazil imeanza kutumia sare ya rangi nyengine.

Mabadiliko haya hivi sasa yamezusha mjadala mkubwa wa kuendelea au kuachana na jezi rangi ya njano? Sare ya njano ilitolewa zabuni na watu zaidi ya 300 walijitokeza kutoa mapendekezo ya muonekano wa hio jezi, kaptula na soksi na namba zitakuwa za maandishi ya aina gani.

Mshindi alikuwa msanifu kijana wa miaka 19, Aldyr Garcia Schlee, kutoka mji wa Pelotas, kusini mwa Brazil ambaye rangi hio ya njano ya sare ilifanana na ile ya dhahabu.

Wakati Brazil ikiwa imepoteza nafasi ya kwanza ya kuwa timu bora duniani, nafasi iliyoishikilia kwa miaka mingi tokea 1970, na kuwa ya tatu ikitanguliwa na Argentina na Ufaransa na kufuatiwa na Ubelgiji mashabiki wa kandanda wa Brazil wanataka rangi ya sare ya timu yao.

Wengi wao wansema rangi ya majano haina tena bahati na taifa lao na kwahivyo ni vizuri kuibadili kama ilivyofanyika miaka ya nyuma.

Hata Rais wa sasa wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva hivi karibuni alisema baada ya miaka 20 ya kukosa kulichukuaa kutafakari kama ipo haja ya kuendelea na sare ya manjano ya dhahabu inayotumika hivi sasa. Hata hivyo, alisema, hayo ni maoni yake na anawaachia wananchi wa Brazil waamue kwa sababu machungu ya kutoutawala ulimwengu wa soka kama ilivyokuwa miaka ya nyuma wanayo wao.

Brazil ilifanya mabadiliko kidogo katika sare yake ya timu taifa mwaka 2020, lakini sio ya kubadili rangi na hii haikuisaidia kurejea kuwa timu bora duniani.

Wapo walioshauri Brazil irudie kutumia sare iliyotumika mwaka 1916 katika mashindano yaliyofanyika Argentina ambapo sare ilikuwa ya njano na kijani (kama Yanga).

Rangi hizi zilikuja kukataliwa baada ya baadhi ya watu kusema hizo ni rangi za taifa na sio vizuri kuzitumia kwa timu ya taifa.

Utafiti wa hivi karibuni umeonyesa wakati katika miaka ya nyuma vijana wengi mitaani walikuwa wanavaa sare ya timu ya Brazil mchana na usiku sasa idadi inazidi kupungua. Sababu ni kwamba hawana tena imani na jezi hio.

Taarifa moja katika vyombo vya habari imeelza kwamba baadhi ya kumbi za muziki zimeanza kuzuwia vijana wanaotaka kuingia kujifurahisha kwa vile wamevaa hiyo sare ya njano ya timu ya Brazil. Sababu ya kufanya uamuzi huo ni kwamba rangi hio ina nuksi na inaweza kuzusha katika ukumbi wa burdani kama inavyoonekana kwa timu ya Brazuil uwanjani.

Baadhi ya watu wa Brazil wanadai kwamba rangi hio ilikuwa na bahati na wachezaji wa zamani kama Pele, Jairzinho, Tostao, Romario, Zico and Ronaldinhio na sio kwa wachezaji wa hivi sasa.

Wapo waliosema kwamba kisirani hicho kilitokana na utawala mbovu wa Rais aliyepita wa nchi hio, Jair Bolsonaro, ambaye wanasema alisababisha nuksi katika kila timu, ikiwa pamoja na michezo kwa vile alitumia rangi hizo katika kampeni ya uchaguzi. Rangi hizo hazikumpa ushindi na hilo sasa linaonekana pia kwa timu ya kandanda ya nchi hio.

Sasa kinachosubiriwa ni kuona uamuzi gani utachukuliwa wa rangi ya jezi ya Brazil. Haya sio madogo, tusubiri makubwa yajayo, mojawapo likiwa je, kubadilika kwa rangi ya sare ya timu hiyo kutaleta mafanikio kama ambayo timu ya kandanda ya nchi hiyo iliyapata miaka ya nyuma? Tusubiri, wakati ndio utatupa jawabu.

Chanzo: Mwanaspoti