Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sarah mwanamke wa Misri anayetamba kwenye soka

Sarah Essam.jpeg Sarah mwanamke wa Misri anayetamba kwenye soka

Thu, 5 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mchezo wa kandanda kwa wanawake unakuwa wa kasi duniani kote, ikiwa pamoja na katika nchi za Kiarabu na Asia na nchi ambazo wanawake (hata watoto) walikuwa hawaruhusiwi hata kufika viwanjani kama watazamaji.

Wachache waliojaribu hapo mwanzo kufika uwanjani, wengine wakiwa wamevalia nguo za kiume ili wasitambulike, walipata mashaka makubwa na kufunguliwa mashitaka ya kukiuka sheria za nchi.

Hivi sasa mchezo huu una mashindano na ligi za soka la wanawake katika nchi 187 na kutoa wachezaji ambao wanalipwa mamilioni ya shilingi, kama ilivyo kwa wachezaji wanaume.

Katika nchi za Kiarabu ambapo wanawake walikutana na vikwazo vingi vya kushiriki na kuangalia michezo wapo kinadada waliopambana kwa ushujaa wa aina yake na kuleta mabadiliko yanayoonekana hii leo.

Wanawake hawa wamekuwa wakitajwa kama ndio waliochapukiza kukua kwa michezo, ikiwemo kandanda, katika nchi zao na ulimwengu wa nchi za Kiarabu na Asia.

Miongoni mwao ni Sarah Essam wa Misri ambaye hivi karibuni alijiunga na klabu ya Stoke City ya Uingereza huku akiendelea na masomo ya uhandisi katika Chuo Kikuu cha Derby, kama walivyofanya kaka zake.

Kabla ya kujiunga na Stoke City alifanya majiribio na klabu za Sunderland, Birmingham na Derby.

Jina la Sarah liligonga vichwa vya habari pale alipokuwa mwanamke wa kwanza wa Misri katika mwaka 2017 kushiriki Ligi Kuu ya Wanawake ya Uingereza huku baadhi ya Wamisri wakimlaani na kumueleza kama mwanamke aliyepotea njia na kuitia aibu Misri. Wakati huo alikuwa na umri wa miaka 16.

Kabla ya hapo alikuwamo katika vikosi vya timu za Misri za watoto wa umri wa chini ya miaka 15 na 17.

Sarah alipenda mchezo wa kandanda tokea akiwa mdogo na kuucheza ndani na nje ya nyumbani yao na kaka zake na majirani.

Mara nyingi alikuwa mwanamke pekee wakati watoto wa mtaani walipokuwa wanacheza kandanda.

Mbali ya kushajiishwa na kaka yake aliyekuwa golikipa maarufu wa timu ya Al Mokawloon walikuwepo kaka zake wa mtaani walioshajiisha na kumfundisha mbinu za kucheza kandanda kwa ustadi.

Mongoni mwao ni mchezaji mashuhuri wa Liverpool na Misri, Mohammed Salah ambaye alikuwa naye katika klabu alizocheza kandanda mtaani kwao.

Salah mpaka leo anao uhusiano mzuri na Sarah ambaye anamueleza kama dada yake mdogo na kipenzi cha familia yao.

Klabu yake ya kwanza kuichezea ni Wadi Degla ambayo ni ya kampuni ya ujenzi na aliisaidia kuwa klabu bingwa mara tatu.

Kutokana na kung’ara akachaguliwa katika timu ya taifa ya Misri iliyokuwa inajitayarisha k wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mnamo mwaka 2016.

Katika mwaka 2017 mwanadada huyu alichaguliwa na Taasisi ya Wanawake wa Kiarabu iliyopo London kama ‘Mwanamke Bora wa Mwaka’ wa nchi za Kiarabu.

Wiki chache ziliopita, akiwa na miaka 24, Sarah alijiunga na timu ya mchezo wa raga kwa wanawake akiwa mchezaji wa kiungo.

“Nililaumiwa sana na marafiki zangu na baadhi ya watu mtaani, lakini kwa vile wazee wangu na kaka zangu waliniambia niendelee na michezo basi sikujali. Nilikuwa na malengo mawili, kuwa mhandisi mzuri na mchezaji kandanda stadi,” alisema Sarah.

Kati ya mafanikio yaliyompoza moyo kwa kuona anaheshimiwa na taifa lake na kimattaifa ni pale alipochaguliwa Balozi wa Shirikisho la Kimataifa la Kandanda (FIFA) kuwa mmoja wa mabalozi wake katika fainali za Kombe la Dunia za Wanaume zilizofanyika Qatar mwaka jana.

Wengine walikuwa wachezaji wa Qatar, Khaled Salman, Mubarak Mustafa, Ibrahim Khalfan, Adel Khamis, Ahmed Khalil, Muhammad Saadoun Al Kuwari, Omans Ali Al Habsi na Mohammed Aboutrika na Wael Jumaa (Misri), Younis Mahmoud (Iraq)David Beckham (Uingereza) , Xavi Hernandez (Hispania), Marcos Evangelista de Morais, marufu kwa jna la Cafu (Brazil, Ronald de Boer (Uholanzi), Samuel Eto’o (Camerron) na Tim Cahill (Australia).

Mfanikio yake makubwa mengine yaliyomuongezea kipato ni kuingia mkataba wa biashara na kampuni maarufu ya vifaa vya michezo, Adidas.

Sarah amesema mafaniko hayo katika kandanda asingeyapata kama wazee wake wasingemshajiisha na kumtaka apuuze lawama za watu wa nje ya familia.

Anatumai baada ya kustaafu kucheza atachukua mafunzo ya mwalimu wa kandanda, lakini pia ataendelea kufanya kazi ya mhandisi.

Viongozi wengi wa michezo wa Uingereza na kwingineko wanaamini mafanikio ya Sarah katika kandanda sio tu yatawashajiisha watoto wa kike wa Misri kupenda soka, bali pia kuwavutia wengine katika ulimwengu wa nchi za Kiarabu.

Kubwa zaidi liliowavutia wataalamu wa soka na mashabiki ni nidhamu ya hali ya juu ya Sarah, iwe ndani na nje ya uwanja wa michezo.

Chanzo: Mwanaspoti