Jadon Sancho ana mtihani mmoja wa kuhakikisha ana kitu cha maana atakachofanya kwenye kikosi cha Manchester United msimu ujao ili awe salama na kupata nafasi katika kikosi hicho cha Kocha Erik ten Hag.
Kocha Ten Hag alikuwa na mazungumzo na kila mchezaji wa Man United kabla ya kuwaruhusu kwenda mapumziko ya kumalizika kwa msimu na Sancho aliambiwa ubora wake ndani ya uwanja ndiyo utakaompa maisha Old Trafford.
Ten Hag anataka kuifanya Man United kuwa timu ya kushindania mataji msimu ujao, hivyo amemwambia Sancho anahitaji mchango mkubwa kutoka kwake, akiamini anafiti kwenye mipango yake.
Sancho mwenye umri wa miaka 23, alinaswa na Man United kutoka Borussia Dortmund kwa ada ya Pauni 73 milioni miaka miwili iliyopita na msimu uliomalizika alikuwa nje ya uwanja kwa miezi mitatu wakati Kocha Ten Hag alipokuwa akimtengeneza awe fiti kimwili na kiakili kabla ya kurejea tena uwanjani Februari.
Ten Hag anaamini wachezaji wake wana uwezo mkubwa wa kupambana na msimu ujao wanaweza kushinda moja ya mataji makubwa kabisa yakayoshindaniwa.
Sambamba na hilo, Man United ipo kwenye mchakato wa kuongeza mastaa wapya kwenye kikosi chake, ikiwamo mastraika na kwenye rada zao wapo Rasmus Hojlund, Harry Kane na Victor Osimhen, huku wakisaka pia huduma ya mabeki wa kati, Axel Disasi na Kim-min Jae ili kuja kufanya Old Trafford kuwa mahali tishio.