Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sancho na ugonjwa wa Man United ambao haueleweki

Sanchozzz (15).jpeg Sancho na ugonjwa wa Man United ambao haueleweki

Sat, 13 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Orodha ni ndefu. Ndiyo. Tuanze na nani? Angel Di Maria halafu kuna Alexis Sanchez halafu kuna Radamel Falcao halafu kuna Paul Pogba, kuna yule Romelu Lukaku. Usimsahau Memphis Depay na Cristiano Ronaldo, lakini pia kuna Donny van de Beek.

Kuna yule Henrikh Mkhitaryan halafu kwa siku za hivi karibuni Waingereza wanajaribu kumuondoa Harry Maguire katika orodha hii, lakini wakati wakipambana kumuondoka sasa hivi jina lililochomoza ni Jadon Sancho.

Nawazungumzia wachezaji waliofeli Manchester United tangu kuondoka kwa Sir Alex Ferguson. Mtu mmoja aliniuliza Manchester United inaumwa ugonjwa gani, lakini mpaka sasa nimekosa jibu sahihi la kumjibu.

Wakati mwingine naamini United inaumwa magonjwa yote. Wamiliki. Makocha. Wachezaji na hadi mashabiki.

Subiri kwanza, katika orodha hii nimemtaja Ronaldo? Ndio. Lakini huyu hakufeli sana uwanjani. Alikuwa mfungaji wao bora katika ujio wake wa pili klabuni hapo.

Alikorofishana na kocha wake, Erik Ten Hag kisha wakafikia uamuzi wa kuagana na Manchester United. Ilikuwa ndoa iliyovunjika kwa huzuni. Mtoto mpendwa ambaye historia yake ilikuwa njema awali lakini ikavurugika wakati ametoka masomoni ughaibuni.

Juzi Sancho naye ameondoka Manchester United. Ameondoka kwa mkopo kwenda klabu yake ya zamani iliyomkomaza Borussia Dortmund. Jaribu kufikiria namna ambavyo Waingereza walitupigia kelele nyingi baada ya Sancho kutamba kule Ujerumani.

Ilionekana kama vile angerudi Manchester akiwa shujaa na nyota ajaye wa England. Hata hivyo haikwenda kama ilivyokwenda. Alirudi kutoka Ujerumani akiwa na namba nyingi za mabao na pasi za mabao. Alipotua United akatuonyesha kiwango duni. Tukamsubiri kwa muda mrefu mpaka tukachoka.

Baadaye akaenda katika vyombo vya habari na kuongea ovyo kuhusu Ten Hag na sasa umekuwa mwisho wa ndoa yao. Walau kwa muda huu.

Tatizo ni yeye au Ten Hag? Nashindwa kuelewa na kuamua kwa sababu katika siku za hivi karibuni United ina matatizo maeneo yote.

Makocha wanaonekana kuwa ni tatizo na wachezaji wanaonekana kuwa ni tatizo. Ni kama ugomvi na Ten Hag na Ronaldo. Ni kama ugomvi wa Jose Mourinho na Pogba. Ni kama tena ugomvi wa Sancho na Ten Hag. Hatujui nani yupo sahihi sana.

Tunachojua ni kwamba United imekuwa ikienda mrama kila uchao. Upande wa makocha wamepita David Moyes, Louis van Gaal, Jose Mourinho, Ole Gunnar Solskjaer, Ralf Rangnick

na sasa Ten Hag. Hakuna aliyeweza kuirudisha United katika hadhi yake.

Ilifikia mahali Jose Mourinho, kocha tuliyemuamini akidai kwamba msimu wake bora zaidi katika soka ni ule alioiwezesha United kushika nafasi ya pili England. Jaribu kufikiria namna tunavyoamini kuwa Mourinho amekuwa na misimu mingi bora ya soka kabla ya kazi yake United.

Na tunaporudi kwa Sancho tunajikumbusha mambo mengi. Cha kwanza tunajikumbusha namna ambavyo United imekuwa kaburi la vipaji vya soka kwa sababu mbalimbali tofauti. Wachezaji wote niliowaorodhesha hapo juu walitajwa kuwa mastaa wakubwa kabla ya kutua Old Trafford.

Walipotua Trafford hakuna aliyeonyesha ubora wa hali ya juu. Labda ni Bruno Fernandes tu ndiye ambaye amekidhi matarajio ya mashabiki wa United. Na hakuja akiwa na jina kubwa kama wenzake kwa sababu alikuwa anatokea katika Ligi Kuu Ureno.

Wengine wengi wamekwenda na maji na kazi yao kubwa imekuwa kupambana kuhakikisha Manchester United inaingia Top Four.

Huu ni mwaka wa 10 Manchester United imekuwa ikipambana kuingia Top Four. Ubingwa wao wa mwisho waliuchukua katika msimu wa mwisho wa Sir Alex Ferguson katika maisha yake ya soka kama kocha.

Zaidi ya kila kitu ni kwamba pesa inaendelea kuteketea Trafford. Na hapa ndipo ninapochanganyikiwa na kujiuliza tatizo la Manchester United. Hata kabla timu haijasogea kwa mmiliki mwingine wa Trafford Bwana Jim Ratcliffe, United ni kati ya timu chache ambazo zimekuwa zina matumizi makubwa ya pesa England na Ulaya kwa ujumla.

Noti zimeteketea United na bado wamiliki familia ya Glazers wamekuwa wakilaumiwa kwa kufeli kwa United miaka ya hivi karibuni. Noti zimeteketea kama ilivyo kwa Manchester City lakini bado pengo baina yao limeendelea kuwa kubwa.

Makocha wamekuwa wakifukuzwa lakini bado pengo limekuwa kubwa. Hata uhamisho huu wa mkopo wa Sancho kwenda Dortmund unaonekana kuwa mtego kwa Ten Hag. United haijaweka kipengele cha kumuuza moja kwa moja.

Inawezekana United wanaamini kwamba Ten Hag anaweza kufukuzwa na Sancho akarudi klabuni hapo chini ya kocha mwingine na kisha akafanya vizuri. Hii ni kwa sababu mpaka sasa hawajui tatizo ni lipi. Kocha au mchezaji?

Vyovyote ilivyo United imeendelea kuumwa ugonjwa usiojulikana. Inazika vipaji vya wachezaji na makocha. Leo sio timu inayoogopwa tena duniani kama ilivyowahi kuwa. Kina Brighton wanakwenda Old Trafford na wanacheza kama wapo nyumbani.

Labda tusubiri kuona Bwana Ratcliffe ataanza kuijenga wapi United. Sancho ni kielelezo kingine cha namna mambo yanavyokwenda kombo Old Trafford. Ukikumbuka namna alivyotua kwa mbwembwe nyingi unabaki mdomo wazi alivyoondoka na kurudi alikotoka.

Nani mwingine atafuata? Hatujui. Tunachojua ni kwamba imeripotiwa kuwa Casemiro hana raha ya kuwepo Manchester United, wakati huohuo Andre Onana anaonekana amekalia kuti kavu. Alikuja na sifa nyingi lakini kila siku anazamisha jahazi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live