Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini England Jadon Sancho anakabiliwa na vita ya kurejesha uungwaji mkono kutoka kwa wachezaji wenzake wa Manchester United pamoja na Kocha, Erik ten Hag baada ya hasira yake ya kuachwa kwenye kipigo cha Ligi Kuu England dhidi ya Arsenal.
Sancho mwenye umri wa miaka 23, alichapisha maneno makali kwenye mtandao wa kijamii akipinga madai ya Ten Hag baada ya kumalizika kwa mechi hiyo akidai aliondolewa kwenye kikosi kutokana na mazoezi yasiyoridhisha, huku mchezaji huyo akikataa maoni hayo yasiyo ya kweli na kusema kupitia X alifanywa ‘mbuzi wa kafara’.
Lakini chanzo kimoja kiliiambia ESPN kuna huruma kidogo kwa Sancho ndani ya chumba cha kubadilishia nguo cha United, kikisema, ‘Wachezaji wenzake wamemchoka.’
Uchezaji wa Sancho mazoezini na siku ya mechi, pamoja na mwenendo wake katika klabu hiyo, umesababisha usajili wa Pauni Milioni 73 kutoka Borussia Dortmund kutokuwa na manufaa.
Licha ya majibu ya haraka ya Sancho kwa maoni ya Ten Hag kwenye mkutano wa waandishi wa habari baada ya mechi dhidi ya Arsenal Sancho hajafuta kauli hiyo.