Mshambulizi wa Chile, Alexis Sanchez ameitakia kila la kheri klabu yake ya zamani ya Arsenal katika mashindano ya Ligi Kuu ya Uingereza msimu wa 2022/23.
Sanchez aliipongeza klabu hiyo ya London, Uingereza wakati wanajiandaa kwa mechi kubwa dhidi ya klabu yake nyingine ya zamani Manchester United katika Uwanja wa Emirates siku ya Jumapili jioni.
Kabla ya mchuano huo unaosubiriwa kwa hamu, Wanabunduki walichapisha video ya maktaba ya mshambuliaji huyo matata akifunga dhidi ya United katika ushindi wao wa 3-0 takriban miaka minane iliyopita.
"Hakuna kuzuia roketi hiyo ya Alexis," Arsenal waliandika chini ya video ambayo ilichapishwa Jumamosi kwenye Instagram.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 34 ni miongoni mwa wanamitandao waliotoa maoni chini ya video hiyo na alishangaa kwamba klabu hiyo ilimkumbuka licha ya uhamisho wake tatanishi kuenda United mwaka wa 2018.
Alichukua fursa hiyo kufunguka kuhusu upendo wake kwa klabu hiyo na kuwatakia kila la heri msimu ukiendelea.
"Mmenikumbuka. Sitawasahau pia. Mtakuwa moyoni mwangu kila wakati, mlikuwa familia yangu ya kwanza Uingereza, na kila mtu alinitunza vizuri haswa mashabiki! kila la kheri wanabunduki!!" aliandika.
Pia alichapisha video hiyo kwenye ukurasa wake na kuandika ujumbe sawa.
Sanchez alikamilisha uhamisho wake wa kwenda kujiunga na Mashetani Wekundu mnamo Januari 2018, hatua ambayo iliwaudhi sana mashabiki wa Arsenal kote duniani ikizingatiwa uhasama kati ya vilabu hivyo viwili.
Raia huyo wa Chile hata hivyo hakuwa na wakati mzuri katika United kama aliokuwa nao akiwa na Wanabunduki huku akifichua baadaye kwamba hakuwahi kuhisi kama amekaribishwa katika klabu hiyo ya Manchester.