Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Samatta na rekodi zake Ulaya

Samatta Mbwana Samatta na rekodi zake Ulaya

Thu, 23 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mshambuliaji wa Tanzania Mbwana Samatta ameiongoza timu yake ya POAK kutwaa ubingwa wa Ugiriki, likiwa ni kombe lake la pili la Ligi Kuu akiwa Ulaya, lakini anaweka rekodi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya pili.

Samatta ambaye ni nahodha wa timu ya Taifa, Taifa Stars anatajwa kama mchezaji mwenye mafanikio makubwa zaidi kuwahi kutokea nchini akiwa ameshazitumikia timu za TP Mazembe, Aston Villa ya Ligi Kuu England pamoja na Genk kwa mafanikio makubwa.

Kitendo cha wikiendi iliyopita timu yake kutwaa ubingwa kinazidi kumweka kwenye daraja lingine la juu la ubora kwenye soka, siyo kwa Tanzania tu bali kwa Afrika Mashariki.

Mafanikio ya mchezaji huyo ambaye aliwahi kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa Afrika kwa wale wanaocheza soka ndani ya bara hili Januari 7, 2016, ni funzo tosha kwa wachezaji wengine wanaochipukia kwa wale ambao wanacheza soka nje na ndani ya nchi.

Wakati anachukua tuzo hiyo alikuwa ametoka kushinda taji la Ligi ya Mabingwa mwaka 2015, ambapo Mazembe walicheza fainali dhidi ya USM Alger na kupata ushindi wa jumla wa mabao 4-1, huku Samatta akifunga katika mechi zote mbili za nyumbani na ugenini.

Tangu Samatta aondoke Afrika hakuna tena mchezaji mwingine wa Tanzania na Afrika ya Mashariki aliyefanikiwa kuchukua tuzo ya mchezaji bora wa Afrika, pia hakuna staa yeyote wa Tanzania aliyewahi kushinda taji la Ligi ya Mabingwa hivyo anaendelea kubaki na rekodi yake.

Sio mara moja kwa Samatta kuweka rekodi na alama mpya katika anga la kimataifa kutokana na ubora anaouonyesha licha ya wengi kuamini kuwa umri umemtupa.

KRC GENK

Siku 28, baada ya kukabidhiwa tuzo ya kuwa mchezaji bora wa Afrika, Samatta alijiunga na KRC Genk akisaini mkataba wa miaka minne na nusu akawa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu Ubelgiji, msimu wake wa kwanza akiwa na timu hiyo alifunga mabao 21 katika mechi 59 za michuano yote.

Msimu wa pili mambo hayakwenda sawa kutokana na majeraha ya mara kwa mara yaliyokuwa yanamuandama, akamaliza na mabao nane katika mechi 35 na asisti nne.

Msimu wa 2018/19, akaongeza uzito baada ya kumaliza akiwa mfungaji bora wa Ligi ya Ubelgiji alipomaliza na mabao 20, akawa mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania kuwahi kuchukua tuzo ya mfungaji bora katika ligi hiyo.

Genk pia ilikuwa bingwa wa Ligi Kuu kwa msimu huo na Samatta akaweka rekodi ya mchezaji wa kwanza wa Tanzania kutwaa ubingwa huo.

Msimu uliofuatia akaweka rekodi nyingi yakuwa mchezaji wa kwanza wa Tanzania kufikisha mabao 50 ya Ligi Kuu Ubelgiji na kucheza kwa mara ya kwanza michuano ya Ligi ya Mabingwa ambapo alifunga bao katika mchezo wa hatua ya makundi kwenye Uwanja wa Anfield wakati timu yake ilipopoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Liverpool.

Hadi sasa ndiye mchezaji pekee raia wa Tanzania kuwahi kufunga bao katika uwanja huo mgumu ambao Jose Mourinho, Sir Alex Ferguson, Patrice Evra na Rio Ferdinand wameutaja kama moja kati ya viwanja vigumu kuwahi kutokea duniani. Atua Villa:

Januari ya mwaka 2020, Samatta alitangazwa kuwa mchezaji wa Aston Villa akitokea Genk na kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu England baada ya kujiunga na timu hiyo kwa miaka mrefu.

Februari 20, 2020 akawa mchezaji wa kwanza wa Tanzania kufunga bao katika Ligi Kuu England dhidi ya Bournemouth, hakuishia msimu huo akacheza fainali ya Carabao dhidi ya Manchester City na kufunga bao lililomwezesha kuweka rekodi nyingine yakuwa mchezaji wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kufanya hivyo, lakini kuwa mchezaji wa kwanza wa Tanzania kufunga bao kwenye Uwanja wa Wembley.

Aenda kwa mkopo

Mambo yalipokuwa magumu Villa alienda kwa mkopo Fenerbahce ambako mwisho wa Msimu wa 2020/21, alisaini mkataba wa kudumu wa miaka minne na nusu, lakini maisha yake hayakuwa mazuri aliandamwa na majeraha ya mara kwa mara na mwisho wa msimu, akatolewa kwa mkopo kwenda Royal Antwerp, kisha Genk na baadaye akauzwa kwenda PAOK ya Ugiriki anakocheza hadi sasa ambapo mkataba wake unamalizika mwakani.

Akiwa huko amekuwa mchezaji wa kwanza wa Tanzania kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu na timu mbili tofauti barani Ulaya. Samatta pia ameweka rekodi yakuwa staa pekee wa Tanzania kufunga kwenye ligi nne barani Ulaya baada ya kuifungia PAOK mabao mawili.

Wanaowania rekodi zake:

Hadi wachezaji wanaoonekana kuwa wana nafasi kubwa ya kuvunja rekodi za Samatta ni Kelvin John ambaye kwa sasa yupo KRC Genk na Novatus Dismas anayeichezea Shakhtar Donetsk ya Ukraine.

Tayari Novatus ameshaifikia rekodi ya kucheza Ligi ya Mabingwa akifanya hivyo na Shakhtar ambapo amekuwa mchezaji wa pili raia wa Tanzania kucheza michuano hiyo, na amechukua ubingwa wa Ligi Kuu Ukraine akiwa na timu hiyo.

Ubingwa aliochukua umemfanya kuwa mchezaji wa kwanza wa Tanzania kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu ya Ukraine, ambapo anahitaji kuchukua taji lingine akiwa na timu hiyo au nyingine ili kumfikia Samatta, lakini akifanikisha hilo bado kuna mengi yanamsubiri kuyavuka ili kumpata Mbwana.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live