Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Samatta anatuachia msala Watanzania

Samatta 681x454.jpeg Samatta anatuachia msala Watanzania

Sun, 14 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zilianza rasmi jana Jumamosi huko Ivory Coast zikishirikisha mataifa 24 ikiwamo Tanzania iliyopangwa Kundi F pamoja na Zambia, Morocco na DR Congo.

Taifa Stars inashiriki fainali hizo kwa mara ya tatu baada ya zile mbili zilizopita za mwaka 1980 na 2019, huku ikiendelea kumtegemea nahodha Mbwana Samatta ‘Samagol’ a.k.a Popat.

Samatta ndiye supastaa na mshambuliaji tegemeo wa timu hiyo, lakini umri unazidi kumtupa mkono na pengine huenda asiwepo katika soka la ushindani miaka michache ijayo.

Kibaya ni kwamba, Samatta anaweza kuondoka akiwa amewaachia msala mashabiki wa soka na soka la Tanzania kwa jumla kutokana na ukweli hadi sasa hajatengenezwa mtu wa kumrithi.

Ndio. Samatta ndiye mshambuliaji tegemeo wa taifa, akiwa ni namba tisa, japo anamudu kucheza kama mshambuliaji namba mbili. Na anaipatia kazi yake uwanjani, ndio maana makocha wote wa timu ya taifa hawajawahi kumuacha kikosini tangu alipoitwa mara ya kwanza.

Hata kama ni ukweli kwamba soka la kisasa linaachana na kumtegemea namba tisa, lakini bado kila timu inahitaji mchezaji atakayekuwa na kazi moja tu ya kutupia mipira kambani kwa kila nafasi itakayotengenezwa uwanjani. Hakuna kocha asiyependa kuwa na straika kama Erling Haaland aliyepo Manchester City au Robert Lewandowski wa Barcelona, hapo ndipo inapoonekana Samatta kama anaiachia nchi msala pale atakapoondoka Stars. Samatta aliyeichezea timui ya taifa jumla ya mechi 75 tangu mwaka 2011 na kuifungia mabao 22, matatu pungufu na aliyonayo Mfungaji wa muda wote, Mrisho Ngassa anatuachia msala kama utani.

Hii ni kwa sababu hakuna mchezaji mbadala wa nafasi yake katika Stars kwa sasa, kwani hata kwenye timu za Ligi Kuu Bara bado hajaonekana mchezaji wa kuchukua nafasi yake.

John Bocco anaelekea ukingoni kwa sasa. Hana tena nafasi kubwa katika timu ya taifa, kwa vile hata katika kikosi cha Simba anayoichezea hana namba.

Yeye ndiye aliyekuwa akiangaliwa kama mbadala wa Samatta, lakini amechemsha mapema. Ni kweli ni mchezaji anayeshikilia rekodi ya kuwa mfungaji wa muda wote wa Ligi Kuu Bara, lakini ile kazi aliyokuwa nayo kwa sasa ni kama haipo, kwani hata anapopewa nafasi ya kucheza uwanjani, mara nyingeni anazingua na kuinyima timu mabao, yaani kifupi Bocco ndio basi tena na huu ni msala.

KELVIN JOHN

Kuna wadau walimuangalia na kumtabiria mshambuliaji chipukizi, Kelvin John ‘Mbappe’ kama ndiye mrithi sahihi wa Samatta. Ilinoga zaidi pale aliposajiliwa na KRC Genk ya Ubelgiji, timu aliyowahi kuitumikia mshambuliaji huyo mkongwe.

Hata hivyo, mambo yamemtibukia mapema. Ameshindwa kufuta nyayo za Samatta. Sio kwa uwanjani tu, hata ile nidhamu ya nje ya uwanja iliyombeba kwa kiasi kikubwa Samatta, nyota huyo chipukizi hana, ndio maana hata kwenye kikosi cha sasa cha Stars kilichopo Ivory Coast hayupo kabisa. Alichomolewa mapema kwa tuhuma za utovu wa nidhamu.

Kama Kelvin aliyekaririwa kabisa anaiga vitu vingi kutoka kwa Samatta kwa ajili ya ndoto zake za kufika mbali kisoka, ameishia njiani, nani wa kumrithi tena Samagol? Huu ni msala!

HABIB KYOMBO

Kuanzia umbo alilonalo na hata uchezaji wake, Kyombo alionekana huenda akawa mrithi sahihi wa Samatta. Ndiye namba tisa halisi miongoni mwa wachezaji waliopo sasa, japo anacheza pia kama winga wakati mwingine au mshambuliaji namba mbili. Bahati nzuri jamaa anajua kufunga, lakini ni kama mtu mwenye homa ya vipindi, yaani ni maji kujaa, maji kupwa. Mechi hii anakupa utamu, lakini mechi ijayo anazingua.

Enzi akiwa Mbao FC jamaa alinoga sana, alikuwa anafunga kila nafasi aliyoipata, akawavutia wengi na kumtabiria kufika mbali, hasa alipoenda kufanya majaribio Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Utamu ulizidi misimu miwili iliyopita aliposajiliwa dirisha dogo na Mbeya Kwanza katika dirisha dogo akitokea Sauzi na kucheza mechi 12 na kufunga mabao sita na kuasisti sita kiasi Simba na Singida zikamgombea.

Pamoja na uwezo alionao, lakini bado haonekani kama anaweza kuwa mrithi wa Samatta kwani hata kwenye timu ya taifa, uitwa kwa nadra na huwa hana maajabu. Huu nao ni msala.

CHARLES ILANFYA

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Mwadui, kisha akatua Simba, baadae akaenda na KMC kabla ya kuibukia Mtibwa Sugar na msimu huu kuichezea Ihefu ambao katika dirisha dogo anarejea Manungu.

Ni mchezaji mwenye nguvu na amejaliwa kasi na anaonekana ni namba tisa ya ukweli kama akituliza akili, japo anaangushwa sana na utovu wa nidhamu ndani ya uwanja. Mara kadhaa Ilanfya amejikuta akilimwa kasi nyekundu kwa matukio anayostaili kufanyiwa yeye na mabeki.

Bado haonekani kama anaweza kumrithi Samatta kwa sasa, kwani hata timu ya taifa ni mara chache amekuwa akiitwa. Hapa bado ni tatizo.

MZIZE AU KACHWELE

Kwa kizazi cha sasa unaweza kumuangalia Clement Mzize wa Yanga au Cyprian Kachwele. Tuanze na Mzize, dogo anajua sana na anaijulia sana namba tisa, japo uzoefu mdogo wakati mwingine unamuangusha, lakini mshambuliaji huyu chipukizi anatia ushawishi kumuamini.

Mzize anajua kutumia nafasi na analazimisha sana mabeki kama alivyokuwa Samatta enzi zake. Ndio maana makocha Nasreddine Nabi na sasa Miguel Gamondi wamekuwa akimtumia na hata timu ya taifa ameitwa mara kadhaa. Kizuri zaidi ana nguvu na kasi na anatumia akili sana uwanjani, kama hafundi basi ujue anampasia mtu atumbukize mpira wavuni. Kama atapigwa tafu na kunyooshwa kidogo ili akae sawa, Mzize anaonekana kwa mbali anaweza kumrithi Samatta, muhimu kuaminiwa.

Kachwele, ambaye safari hii yupo kwenye kikosi cha Stars kilichopo Afcon. Dogo huyo alikuzwa na Azam FC kabla ya sasa kuuzwa Canada kwenye klabu ya Vancouver Whitecaps.

Ni mchezaji mwenye utulivu wa akili akiwa langoni. Alionekana kwenye Ligi ya Vijana U20 akiwa na Azam ambapo dogo alikuwa anafunga sana. Anajua kujipanga na kutumia nafasi, na pia anakaa kwenye eneo sahihi. Akiandaliwa vyema huenda msala anaotuachia Samatta utaondoka.

WENGINE NAO

Sio kama hakuna namba tisa wakali nchini, hapana! Ni vile tu wenyewe hawajui kutumia nafasi zao. Wapo Daruwesh Saliboko na Wazir Junior wa KMC ni washambuliaji kwelikweli, lakini ni ngumu kuwawekea dhamana, kwani hawachelewi kukuangusha. Yupo pia Matteo Antony na Seif Rashid Karihe wanaokipiga Mtibwa Sugar. Nao sio wachezaji wa kubezwa, lakini bado hawakupi kile unachotarajiwa kutoka kwao na hilo ni tatizo linalokatisha tamaa kama ilivyo kwa washambuliaji wengine wanaozitumikia timu tofauti za Ligi Kuu na hata Championship.

 NINI KIFANYIKE?

Hapa chini ni nyota wa zamani wa soka nchini baadhi wakiwa wametumika kama washambuliaji wa mwisho wa timu walizocheza, wametoa maoni na mitazamo juu ya tatizo la kukosekana kwa washambuliaji wa kuaminika.

Staa wa zamani wa Yanga, Abeid Mziba ‘Tekero’, anasema: “Sioni mshambuliaji, wengi wameshindwa kupambania nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza wamekuwa wakiridhika kuwa kwenye timu kubwa bila kupambana na kuonyesha viwango vya juu. Hawa kina Sopu na Mzize wanatakiwa kuonyesha na sio vinginevyo,” alisema Tekero.

Naye Sekilojo Chambua aliyewika na Tukuyu Stars, Yanga na Taifa Stars anasema ni vizuri klabu za Ligi Kuu kuwa na mipango endelevu ya kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana ambavyo vitakuwa msaada kwa taifa kuliko kuwekeza nguvu kubwa kwa wachezaji wa kigeni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live