Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Samatta akaribia rekodi mpya Ulaya

Mbwana Samatta Debut Mbwana Samatta

Sat, 26 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Hearts juzi umeiweka timu ya Mbwana Samatta, PAOK Thessaloniki katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya makundi ya mashindano ya Europa Conference League ikihitaji sare tu au ushindi katika mechi ya marudiano nyumbani ili isonge mbele.

Samatta amesajiliwa na PAOK katika dirisha kubwa la usajili linaloendelea la majira ya kiangazi akiwa mchezaji huru baada ya kuvunja mkataba wake na Fenerbahce ya Uturuki.

Wakati PAOK ikikaribia kutinga hatua hiyo, Samatta anakaribia kuweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza hatua ya makundi ya mashindano matatu makubwa ya klabu kwa bara la Ulaya yanayosimamiwa na Umoja wa Vyama vya Mpira wa Miguu barani humo (Uefa).

Nyota huyo wa zamani wa Simba na TP Mazembe, tayari alishafanikiwa kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini pia amewahi kuonja ladha ya hatua ya makundi ya mashindano mengine ya soka kwa ngazi ya klabu barani humo ya Europa League.

Samatta alicheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika msimu wa 2019/2020 akiwa na Genk ya Ubelgiji ambapo ilipangwa kundi E ikiwa na timu za Liverpool, Napoli na RB Salzburg ikimaliza mkiani ikiwa imekusanya pointi moja.

Katika hatua hiyo ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huo, Samatta hakumaliza kinyonge kwani alipachika mabao matatu.

Mashindano ya Europa League amecheza mara tatu akiwa na timu nne tofauti ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni katika msimu wa 2016/2017 akiwa na Genk ambapo waliishia hatua ya robo fainali na kisha msimu wa 2018/2019 akiwa na timu hiyohiyo walipoishia katika hatua ya 32 bora na mara nyingine ni msimu wa 2021/2022 akiwa na Fenerbahce pamoja na Royal Antwerp ambapo iliishia hatua ya makundi.

Ikumbukwe katika mashindano hayo ya Europa League, Samatta amefunga idadi ya mabao nane katika mechi 25.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live